Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameridhishwa na hatua za utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Gesi Asilia la inchi 14 kutoka Kisima cha Ntorya hadi Madimba mkoani Mtwara ambao umefikia asilimia 78 huku ukitarajiwa kukamilika februari 2027.
Mhe. Ndejembi ameeleza hayo leo, Novemba 13, 2026, wakati wa ziara yake mkoani Mtwara, alipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi huo utakaowezesha kusafirisha rasilimali ya gesi asilia kutoka eneo la ugunduzi la Ntorya hadi katika kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba ili kuweza kutumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme, majumbani, vyombo vya usafiri n.k
Amesema takribani Shilingi bilioni 119 zilizotumika katika mradi huo ni fedha za ndani, bila kutegemea ufadhili wa nje, hatua inayoonesha uwezo wa nchi kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa kutumia rasilimali zake.
Amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususan mkoani Mtwara ambako kuna miundombinu ya kusambaza gesi majumbani. Vilevile, gesi hiyo itatumika katika sekta ya usafirishaji na kuongeza thamani ya rasilimali za gesi asilia kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa Taifa.
Ameongeza kuwa, kwa sasa viwanda 48 nchini vinatumia gesi asilia katika shughuli zake za uzalishaji.
Mhe. Ndejembi amepongeza Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha nchi inakuwa na miundombinu yake ya uzalishaji, usafirishaji na uchakataji wa gesi asilia.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba ameshiriki katika ziara hiyo akiongoza watendaji kutoka Wizara ya Nishati na TPDC.






No comments:
Post a Comment