Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Nishati ya Tanzania na Malawi imekutana kujadili uwezekano wa kujenga bomba la kusafirisha mafuta kutoka Mkoa wa Songwe nchini Tanzania hadi Malawi.
Majadiliano hayo yamefanyika leo, Novemba 13, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati, Dar es Salaam, ambapo ujumbe wa Malawi umeongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Nishati, Joseph Kalowekamo, huku ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Kamishna Msaidizi wa Petroli (Mkondo wa Kati na Chini), Grace Mwakasege. Kikao hicho pia kimewashirikisha wataalamu kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Akizungumza katika kikao hicho, Kalowekamo amesema Malawi inategemea kwa zaidi ya asilimia 70 bandari za Dar es Salaam na Tanga kuingiza mafuta, ambayo husafirishwa kwa malori umbali wa zaidi ya kilomita 1,500 hadi nchini humo.
Amesema hali hiyo muda mwingine hupelekea ucheleweshaji wa huduma na changamoto nyinginezo za usafirishaji, hivyo nchi hiyo inaona umuhimu wa kuangalia uwezekano wa kutumia bomba la mafuta kutoka Songwe hadi Malawi ili kurahisisha usafirishaji na kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa mafuta.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwakasege amesema Tanzania na Zambia zipo katika hatua za awali za maandalizi ya mradi wa ujenzi wa Bomba jipya la Mafuta la TAZAMA, ambapo upembuzi yakinifu wa mradi na tathmini ya soko zimezingatia mahitaji ya nchi washirika wa karibu, zikiwemo Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ameeleza kuwa, kwa kuzingatia mahitaji ya Malawi, kuna uwezekano wa nchi hiyo kuunganishwa na Bomba Jipya la TAZAMA kupitia mojawapo ya vituo vya kutolea mafuta vinavyotarajiwa kujengwa katika Mkoa wa Songwe, jambo litakalowezesha Malawi kunufaika na miundombinu hiyo kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa mafuta.
Majadiliano hayo ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano wa sekta ya nishati kati ya Tanzania na Malawi, kufuatia makubaliano ya ushirikiano yaliyofikiwa na nchi hizo mwaka 2023. Nchi hizo, ambazo pia ni wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), zimekuwa zikiimarisha mashauriano kupitia mikutano ya Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara za Nishati kwa lengo la kubaini maeneo ya pamoja ya uwekezaji na maendeleo ya sekta hiyo.
Mradi wa Bomba Jipya la Mafuta la TAZAMA unatokana na maelekezo ya Marais wa Tanzania na Zambia yaliyotolewa katika kikao chao cha Oktoba 2023, ambapo Wizara za Nishati za nchi hizo ziliagizwa kuanza maandalizi ya mradi huo.
Bomba hilo linatarajiwa kuwa na vituo vya kutolea mafuta katika maeneo ya Morogoro, Makambako, na Songwe kwa upande wa Tanzania, pamoja na Mpika na Serenje kwa upande wa Zambia.






No comments:
Post a Comment