
NA SHUA NDEREKA, OKULY BLOG, MOROGORO
Mkoa wa Morogoro unatarajia kufanya maonesho makubwa ya biashara na uwekezaji yanayojulikana kama Morogoro Region Trade Exhibition (MORO EXPO 2026), yakilenga kufungua fursa mpya za kibiashara, kukuza ubunifu na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amesema maonesho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa vitendo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuijenga Tanzania yenye uchumi imara na shindani wenye thamani ya dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Kilakala amesema maonesho hayo yanatarajiwa kuwa endelevu kwa kufanyika kila mwaka, yakitoa jukwaa kwa wafanyabiashara kuonesha bidhaa na ubunifu wao, kupanua wigo wa masoko pamoja na kujenga fursa za uwekezaji zinazoweza kuvutia mitaji kutoka ndani na nje ya nchi.
“Umuhimu wa maonesho ya MORO EXPO 2026 ni kuwa jukwaa la kuonesha bidhaa, huduma na ubunifu katika sekta za biashara, viwanda, kilimo, utalii, madini, uvuvi na ufugaji. Hivyo, ushiriki wenu wafanyabiashara utakuza uchumi katika mkoa,” amesema Kilakala.
Naye Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya MORO EXPO, Dastan Mziwanda, amesema maonesho hayo yamelenga kukuza shughuli za biashara, kufungua fursa za masoko kwa wafanyabiashara na kuvutia uwekezaji katika Mkoa wa Morogoro.
Amesema Mkoa wa Morogoro una utajiri mkubwa wa fursa za kiuchumi na uwekezaji zinazopaswa kuendelezwa na kutumika kikamilifu, ukiwa na utajiri wenye thamani ya shilingi trilioni 11.4 kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) hadi kufikia Juni 2026.
“Mkoa wa Morogoro ni wa nne, ambapo Mkoa wa Dar es Salaam una trilioni 39.8, ukifuatiwa na Jiji la Mwanza lenye trilioni 16.7 na Mkoa wa Mbeya wenye trilioni 12.9,” amesema Mziwanda.
Kwa upande wake, Said Kimweri, mfanyakazi wa Nanguji Memorial Hospital iliyopo Manispaa ya Morogoro, amesema wananchi watakaotembelea maonesho hayo watanufaika na huduma za upimaji wa afya bila malipo, zitakazojumuisha uchunguzi wa meno, macho, moyo na mapafu.
Maonesho ya MORO EXPO 2026 yanatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 23 hadi 27 mwaka huu katika kituo cha zamani cha daladala manispaa ya Morogoro, yakiwa jukwaa la kuwakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara kwa lengo la kujenga mitandao ya kibiashara na kukuza uhusiano ndani na nje ya Morogoro.
Kauli mbiu ya maonesho hayo kwa mwaka huu ni: “Kukuza biashara, uwekezaji na viwanda kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Morogoro.”


No comments:
Post a Comment