WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka tume za uchaguzi za nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutumia ipasavyo teknolojia, mitandao ya kijamii na akili unde (AI) katika kuboresha usimamizi wa uchaguzi na kuimarisha demokrasia katika ukanda huo.
Dkt. Mwigulu amesema matumizi ya teknolojia za kisasa yana nafasi kubwa katika kuboresha mawasiliano, kutoa elimu kwa wapiga kura na kusambaza taarifa zinazohusu michakato ya uchaguzi kwa wakati, akisisitiza umuhimu wa kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia hizo ikiwemo usambazaji taarifa potofu.
“Kwa kuwa uchaguzi ni zoezi lenye hamasa kubwa kwa jamii, taarifa zisizo sahihi zinaposambazwa kwa kasi zinaweza kuwa na athari hasi na hata kusababisha migawanyiko katika jamii, kuathiri taswira ya taasisi za uchaguzi na kupunguza imani ya wananchi katika michakato ya kidemokrasia," amesema Dkt. Mwigulu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba 23, 2026) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 28 wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi za Nchi Wanachama wa SADC (ECF-SADC), katika hoteli ya Hyatt Regency - The Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa siku tatu unajadili usimamizi wa uchaguzi katika zama za mitandao ya kijamii na namna ya kuimarisha wajibu wa taasisi za usimamizi wa uchaguzi katika ukanda huo, ambapo Dkt. Mwigulu amesema mitandao ya kijamii imekuwa chanzo muhimu cha taarifa kwa wananchi wengi, hususan vijana, kutokana na uwezo wake wa kusambaza habari kwa haraka.
Amezitaka tume hizo kuendelea kujenga uwezo katika matumizi ya akili unde (AI), akieleza kuwa teknolojia hiyo inaendelea kukua na kubadilika kwa kasi, hivyo ni muhimu kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zake na kutumia fursa zinazotokana na maendeleo yake.
“Ni vyema mkaweka mikakati ya kukabiliana na changamoto za matumizi yake na kuona namna ya kutumia fursa ambazo zinaweza kupatikana kutokana na kuimarika zaidi kwa mifumo yake,” amehimiza Waziri Mkuu.
Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa usimamizi imara wa uchaguzi ni msingi muhimu wa kukuza demokrasia na ustawi wa jamii, hivyo amezitaka nchi za SADC kuendelea kuimarisha mifumo ya uchaguzi inayozingatia sheria, kanuni na misingi ya kidemokrasia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania - Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema ushiriki wa Tanzania katika ECF-SADC tangu kuanzishwa kwake mwaka 1998 umeiwezesha nchi kupata fursa za kujifunza na kubadilishana uzoefu na tume nyingine za uchaguzi katika ukanda huo kwani ushirikiano huo umesaidia kuimarisha mifumo ya uchaguzi na kujenga uwezo wa taasisi za usimamizi wa uchaguzi.
Naye, Rais wa Jukwaa la ECF-SADC, Jaji Dkt. Manuel Pereira da Silva, amesema jukwaa hilo lina jukumu la kuimarisha uhuru, kutopendelea upande wowote na kukuza weledi wa taasisi za usimamizi wa uchaguzi katika nchi wanachama pamoja na kujifunza mbinu mpya za usimamizi wa uchaguzi na kujenga mahusiano ya kikazi hata katika vipindi ambavyo nchi hazipo kwenye uchaguzi.
Mkutano huo wa 28 wa ECF-SADC umewakutanisha viongozi mbalimbali wakiwemo wenyeviti, makamishna, wakurugenzi na watendaji wa tume za uchaguzi kutoka nchi wanachama wa SADC, ukiwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa uchaguzi, changamoto za teknolojia na nafasi ya mitandao ya kijamii katika michakato ya kidemokrasia.







No comments:
Post a Comment