Na: OWM–TAMISEMI, Tanga
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ametembelea na kukagua miradi ya TACTIC yenye thamani ya Shilingi Bilioni 36 inayotekelezwa jijini Tanga.
Uboreshaji wa miundombinu ya masoko, eneo la mapumziko ya ufukweni, barabara na mifereji ya maji ya mvua, pamoja na ujenzi wa ofisi za wahandisi wa Jiji la Tanga na TARURA, ambapo utekelezaji wake umefikia wastani wa asilimia 65.
Prof. Shemdoe ametembelea miradi hiyo Novemba 18, 2026, kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wake na kuhimiza wakandarasi kukamilisha kazi kwa kuzingatia masharti ya mikataba. Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi hiyo jijini Tanga.
“Nimetembelea mradi wa ujenzi wa ofisi ya wahandisi wa Jiji na TARURA uliofikia asilimia 65, mradi wa uboreshaji wa eneo la mapumziko ya ufukweni Raskazone uliofikia asilimia 65, ujenzi wa Soko la Makorora uliofikia asilimia 65, Barabara ya Tangasisi iliyofikia asilimia 65, Barabara ya Magomeni iliyofikia asilimia 80, pamoja na mfereji wa maji ya mvua wa Kange–Mwarongo wenye urefu wa kilomita 10 ambao umefikia asilimia 65,” ameeleza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amewataka Wakuu wa Mikoa inayotekeleza miradi ya TACTIC kuongeza juhudi katika usimamizi na ufuatiliaji wa miradi hiyo, akieleza kuwa baadhi ya mikoa aliyotembelea Makamu wa Rais imeonesha kiwango cha chini cha utekelezaji. Amewataka viongozi wa Mkoa wa Tanga kuongeza kasi ya usimamizi wa miradi hiyo licha ya kufikia asilimia 65, ikilinganishwa na asilimia 77 iliyotarajiwa kufikiwa katika hatua hii ya utekelezaji.
“Mhe. Rais ametoa fedha hizi si kwa ajili ya wakandarasi kuwepo katika maeneo ya miradi, bali ni kwa ajili ya kusogeza na kuboresha huduma kwa Watanzania. Hivyo, namtaka mkandarasi kuongeza kasi na ufanisi wa kazi, kwani hakutakuwa na nyongeza ya muda wa utekelezaji wa mradi,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Miradi hiyo ya TACTIC jijini Tanga inatekelezwa na wakandarasi wakiwepo M/s Jiangx pamoja na Salem Construction Ltd, na kampuni za ushauri UWP na STET.






No comments:
Post a Comment