TANZANIA YAUNGA MKONO MAPENDEKEZO YA EAC KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA WA KANDA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 21, 2026

TANZANIA YAUNGA MKONO MAPENDEKEZO YA EAC KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA WA KANDA


Tanzania imeunga mkono mapendekezo ya kuimarisha ushirikiano wa ulinzi na usalama miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikisisitiza umuhimu wa maamuzi ya kimkakati yatakayosaidia kukabiliana na vitisho vya kiusalama na kudumisha amani na utulivu katika ukanda huo.

Hayo yamejiri katika Mkutano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri kuhusu Ushirikiano katika Masuala ya Ulinzi uliohitimishwa jijini Kampala, Uganda, Novemba 20, 2026, huku ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Meja Jenerali Michael Mumanga kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mkutano huo ulijadili mikakati ya kukabiliana na vitisho vinavyoikabili Afrika Mashariki, vikiwemo migogoro ya kivita, itikadi kali zenye misimamo ya vurugu, vitisho vya usalama baharini, uhalifu wa mtandaoni na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Akifungua mkutano huo, Waziri wa Nchi wa Ulinzi na Masuala ya Maveterani wa Uganda, Mhe. Oleru Huda Abason alisisitiza umuhimu wa maamuzi yanayozingatia maslahi ya wananchi wapatao milioni 300 wa EAC, akieleza kuwa amani na usalama ni msingi muhimu wa maendeleo ya Jumuiya.

Alibainisha kuwa changamoto za kiusalama katika ukanda huo zinavuka mipaka ya nchi, hivyo zinahitaji ushirikiano wa pamoja badala ya kila nchi kukabiliana nazo kivyake.

Katika kuimarisha ushirikiano huo, wajumbe walijadili hatua mbalimbali, zikiwemo kuendesha mazoezi ya pamoja ya kijeshi, kutekeleza Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja, kuboresha elimu na mafunzo ya kijeshi na kuimarisha huduma za afya kwa majeshi ya nchi wanachama.

Mapendekezo hayo yakitekelezwa yanatarajiwa kuongeza uwezo na utayari wa majeshi ya nchi wanachama kukabiliana na vitisho vya kiusalama, huku yakiweka msingi imara wa kulinda amani na utulivu katika Afrika Mashariki.






No comments:

Post a Comment