Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema hatua kuu za kiutaratibu katika kesi iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Tundu Lissu zilifanyika kwa kuzingatia mfumo wa sheria za mwenendo wa makosa ya jinai, huku ikisisitiza kuwa uzingatiaji wa taratibu hizo pekee hauondoi wajibu wa kulinda haki za msingi za binadamu.
Katika tamko lake la Novemba 13, 2026, kuhusu masuala ya haki za binadamu na utawala bora yaliyojitokeza katika kesi hiyo THBUB imeeleza kuwa tathmini yake ilibaini hatua kuu za kesi zilizothibitishwa na kumbukumbu ilizozichunguza zilifuata mfumo wa kisheria uliowekwa.
THBUB imeeleza imesisitiza kuwa kufuata taratibu za kukamatwa, kufikishwa mahakamani na kusikilizwa kwa kesi hakutoshi peke yake kuthibitisha kuwa haki zote za binadamu zililindwa kikamilifu.
Tume imetaja umuhimu wa kuhakikisha mtuhumiwa anapata msaada wa kisheria, muda na mazingira ya kutosha kuandaa utetezi, nyaraka muhimu za kesi na nafasi ya kuwauliza maswali mashahidi.
Katika eneo la haki za watu walioko kizuizini, THBUB imeeleza kuwa ilifanya uchunguzi wake Juni 27, 2025 kuhusu madai ya namna Lissu alivyotendewa alipokuwa kizuizini ambapo imesema uchunguzi huo ulibaini kuwa katika kipindi kilichofanyiwa tathmini Lissu alikuwa akipata haki ya kuabudu, faragha, kuwasiliana na wakili au rafiki pamoja na kufanya mazoezi ya mwili.
Pamoja na matokeo hayo, Tume imesisitiza kuwa mamlaka za magereza zina wajibu endelevu wa kuheshimu na kulinda utu na haki za msingi za watu wote walioondolewa uhuru wao.
Aidha, Tume hiyo imesema haikubaini ushahidi uliothibitishwa wa ubaguzi dhidi ya Lissu au kukosekana kwa uwazi wa kiutaratibu katika hatua za kesi ilizozichunguza.
Hata hivyo, THBUB imeweka wazi kuwa haichukui upande wa kuunga mkono au kupinga hukumu ya Lissu wala haina mamlaka ya kutathmini upya ushahidi, kubatilisha hukumu au kuingilia uamuzi wa Mahakama.
Imesisitiza kuwa kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama kunapaswa kushughulikiwa kupitia njia za kisheria ikiwemo rufaa huku mijadala ya umma kuhusu maamuzi ya Mahakama ikiendelea kufanyika kwa kuzingatia uhuru wa Mahakama na utawala wa sheria.
Tume imesisitiza kuwa ulinzi wa haki za binadamu, uhuru wa Mahakama, utawala wa sheria na uwajibikaji wa taasisi ni nguzo zinazotegemeana katika kuimarisha utawala wa kikatiba nchini.


No comments:
Post a Comment