WATHIBITI UBORA WA SHULE 160 WAPATIWA MAFUNZO YA UONGOZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 28, 2026

WATHIBITI UBORA WA SHULE 160 WAPATIWA MAFUNZO YA UONGOZI

BAGAMOYO, 28 Novemba, 2026

Wathibiti ubora wa shule 160 kutoka mikoa ya Mtwara, Pwani, Kilimanjaro, Dodoma na Tanga wamehitimisha mafunzo ya siku tatu ya uongozi, usimamizi wa shule na utawala bora katika elimu, yaliyofanyika kuanzia Novemba 26 hadi 28, 2026 ADEM, Bagamoyo.

Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Uthibiti Ubora, Dkt. Ephraim Simbeye, Mkurugenzi Msaidizi wa Uthibiti Ubora kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bw. Edward Wawa, alisema mafunzo hayo yameandaliwa ili kuongeza weledi, ubora na tija katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Jukumu letu la uthibiti ubora ni kuhakikisha viongozi wa shule wanazingatia miongozo iliyowekwa ili kufikia azma ya Serikali ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji. Lengo ni kila mwanafunzi apate elimu bora kama inavyoelekezwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na Mwongozo wa Uthibiti Ubora wa Shule wa mwaka 2017 toleo la 2024," alisema Bw. Wawa.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka na yanaenda kuongeza tija, huku akisisitiza: "Ni lazima muwe waadilifu; taarifa mnazokusanya na ushauri mnaoutoa uwe wa kweli, wa haki na unaotokana na ushahidi ili mfumo wetu uendelee kuaminika. Tusikome kujifunza mambo mapya, tutumie teknolojia na tushirikiane kwa karibu na walimu, uongozi wa shule, wanafunzi, wazazi na wadau wote wa elimu."

Bw. Wawa alihitimisha kwa kuwakumbusha washiriki umuhimu wa kazi yao kuzaa matokeo chanya darasani: "Jambo la msingi ni kuhakikisha kazi tunayoifanya inaleta matokeo yaliyokusudiwa na kumsaidia mwanafunzi kujifunza vizuri ili afikie malengo yake."

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid, alisema taasisi hiyo imehakikisha washiriki wanajengewa umahiri katika uongozi, usimamizi na utawala wa shule, utawala bora katika elimu, itifaki, usimamizi wa utekelezaji wa Mpango wa Jumla wa Maendeleo ya Shule, ubora wa utekelezaji wa mtaala, ustawi na usalama wa walimu na wanafunzi, pamoja na utafutaji na usimamizi wa rasilimali za shule, sambamba na vigezo vya upimaji wa ubora shuleni.

Naye Mwenyekiti wa Washiriki, Mwl. Albert Mtalemwa, aliishukuru Serikali kwa kuwajengea uwezo na kuahidi kuwa wataenda kutumia elimu hiyo kwa vitendo ili thamani ya fedha iliyotumika ionekane na lengo la kuinua ubora wa elimu nchini litimie.

Mafunzo hayo yamefadhiliwa na mradi wa BOOST kupitia Afua namba 8 inayolenga kuimarisha uongozi na usimamizi wa shule, ikiwa ni muendelezo wa mafunzo yaliyokwisha kutolewa kwa walimu wakuu, maafisa elimu kata, halmashauri na mikoa nchini ili kujenga uelewa na usimamizi wenye uwiano sawa.

No comments:

Post a Comment