Na Boniphace Epimack, OKULY BLOG – DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ametangaza kufanyika kwa Mbio za Hisani za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Charity Run) zitakazofanyika Novemba 28, 2026, jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya Jukwaa la Sita la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 23, 2026, jijini Dodoma, Mhe. Senyamule amesema mbio hizo zitaanzia na kuhitimishwa katika Uwanja wa Jamhuri, kuanzia saa 11:30 alfajiri hadi saa 1:30 asubuhi, huku washiriki wakipita katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na Stesheni ya Reli ya Kisasa ya SGR Samia Suluhu Hassan.
Amesema lengo kuu la mbio hizo ni kuchangisha fedha zitakazokuwa mtaji wa kuanzisha Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Basket Fund – NBF), unaolenga kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje ya nchi na kuimarisha uwezo wa kifedha pamoja na uendelevu wa mashirika hayo yanayotoa huduma muhimu kwa wananchi, hususan katika ngazi za jamii.
“Mbio hizi si mbio za kawaida. Kila mtu aliyesajiliwa na kushiriki atakuwa amechangia moja kwa moja katika mfuko huo. Hata yule ambaye hataweza kushiriki mbio anaweza kuchangia fedha au vifaa ili kuwezesha uendelevu wa mfuko huu,” amesema Mhe. Senyamule.
Amesisitiza kuwa sekta imara ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali inachangia kujenga familia imara, jamii imara na Taifa imara, akieleza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya Taifa.
Mbio hizo ni sehemu ya Jukwaa la Sita la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 2026, linaloandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO).
Jukwaa hilo litafanyika kuanzia Novemba 25 hadi 28, 2026, jijini Dodoma, likiwa ni la sita tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021. Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Kaulimbiu ya jukwaa la mwaka huu ni “Fikra Mpya Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani.”
Kwa mujibu wa Mhe. Senyamule, kaulimbiu hiyo imezingatia changamoto zinazokabili sekta hiyo, zikiwemo utegemezi wa ufadhili kutoka nje, masharti magumu ya upatikanaji wa fedha na kutotabirika kwa vyanzo vya ufadhili. Hivyo, jukwaa hilo linatoa fursa ya kujadili mikakati mipya ya kupata rasilimali za ndani ili kuhakikisha mashirika hayo yanaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa uendelevu.
Jukwaa hilo linatarajiwa kuwakutanisha takribani washiriki 3,500 kutoka makundi mbalimbali, yakiwemo wawakilishi wa Wizara, Idara na Taasisi za Kisekta, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, vyombo vya habari, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wanufaika wa miradi na afua zinazotekelezwa na mashirika hayo.
Akizungumzia maandalizi ya tukio hilo, Mhe. Senyamule amesema Mkoa wa Dodoma umefarijika kupata heshima ya kuwa mwenyeji wa jukwaa hilo la kitaifa, akibainisha kuwa hadhi ya Dodoma kama Makao Makuu ya nchi inaendelea kuimarisha nafasi yake katika kuandaa mikutano mikubwa, maonesho na shughuli mbalimbali zinazowakutanisha wananchi.
“Tukio hili linaiweka Dodoma katika ramani ya mikutano mikubwa ya kitaifa na ni fursa ya kiuchumi kwa sekta za hoteli, pamoja na usafiri na usafirishaji,” amesema.






No comments:
Post a Comment