Polisi mkoani Kilimanjaro imesema binti huyo hakutekwa nyara kama ambavyo wanafamilia walitoa taarifa Kituo cha Polisi Himo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema jana kuwa uchunguzi uliofanywa umethibitisha kuwa bibi harusi huyo hakuwa ametekwa nyara.
“Polisi walifungua jalada la uchunguzi na ilibainika kuwa taarifa za kutekwa zilizokuwa zimetolewa hazikuwa na ukweli, bali aliondoka kwa kupanda pikipiki,” alisema.
Kamanda Ngonyani alisema uchunguzi huo ulibaini kuwa wakati akipambwa, aliomba kwenda kujisaidia na baadaye kuomba apelekewe kanga na ‘tishu’ lakini akatumia mwanya huo kuondoka,” alisema.
Alisema uchunguzi huo umebaini kuwa baada ya kupanda pikipiki ilimpeleka hadi kituo cha mabasi na alimlipa dereva wa bodaboda kisha alipanda gari la abiria lililompeleka hadi mjini Moshi.
Tukio hilo lilitokea Jumamosi iliyopita saa 6.30 mchana eneo la Lole huko Mwika, Moshi wakati bibi harusi huyo alipotoroka saluni akimwacha mpambe wake akiendelea kupambwa.
Ndoa hiyo ilikuwa ifungwe saa tisa alasiri katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Lole Dayosisi ya Kaskazini na baadaye sherehe ingefanyika katika Ukumbi wa Mamba Complex.
Habari zilizopatikana jana kutoka kwa familia ya Machange, zilieleza kuwa Doroth alipatikana juzi baada ya kuonekana akiweweseka, kisha akapelekwa hospitali ya Seliani kwa matibabu.
Ndugu wa karibu wa familia ya Machange ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alisema kulikuwa na kikao kilichokuwa kikiendelea kati ya familia ya Machange na Msuya.
“Jana (juzi) tulipigiwa simu na kuelezwa kuwa Doroth amepatikana Arusha lakini yuko kama hajielewielewi na hajui nini kimetokea,” alisema.
Habari zaidi kutoka ndani ya familia hiyo, zinadai kuwa bibi harusi huyo alikuwa ametaka harusi hiyo iahirishwe na ombi hilo alilitoa zaidi ya mara 10 bila kueleza sababu.
No comments:
Post a Comment