Akiwa kwenye kampeni za kuutaka urais kwa tiketi ya CCM, alisema ataanza kazi mara baada ya kuapishwa, na atafanya kazi usiku na mchana.
Katika siku nne za kwanza, Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano pia ametoa maagizo kadhaa, ikiwemo kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuhakikisha inakusanya kodi hasa kwa kuwabana wafanyabiashara wakubwa, kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kutangaza elimu bure kuanzia mwakani.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo baada ya kufanya kikao na makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade kwa lengo la kutoa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Alisema mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi huko nje, ndiyo watakaotakiwa kufanya shughuli zote kwenye nchi wanazofanya kazi hadi hapo atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine.
Wasemavyo wasomi
Wengi waliozungumza na gazeti hili walimsifu Rais Magufuli kutokana na kuagiza walipa kodi, hasa wafanyabiashara wakubwa wadhibitiwe, kusimamisha safari za nje, wakisema fedha zitakazookolewa zitasaidia katika kutekeleza ahadi ambazo yeye na chama chake walizitoa wakati wa kampeni.
“Ingawa kitaalamu huwezi kupima utendaji kwa siku tatu, Rais Magufuli ameanza kazi kwa kutoa maagizo ili kuhakikisha anatekeleza aliyoahidi kama kutoa elimu bure ya msingi hadi sekondari,” alisema Profesa Lugano Kusiluka wa Chuo Kikuu Huria (OUT).
“Sasa ni wajibu wa watendaji wa serikali kutekeleza.”
Sifa kama hizo zilitolewa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Charles Marwa, ambaye alisema hatua ya kuanzia kuwabana walipa kodi wakubwa ni mwanzo mzuri, akishauri Dk Magufuli aanze kuwabana maafisa wa juu wa TRA ndipo ashuke kwa maafisa wa chini kudhibiti kodi.
Suala la kodi pia lilizungumziwa na Dk Alexander Makulilo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye alisema baadhi ya wafanyabiashara wakubwa ndiyo wakwepaji wakubwa wa kodi.
“Wakati wafanyakazi wenye mishahara mikubwa ndiyo wanaolipa kodi kubwa serikalini, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa ndiyo wanaoongoza kukwepa na kusamehewa kodi,” alisema.
Alitaka juhudi kubwa ifanyike katika kuhakikisha wafanyabiashara hao hawakwepi kodi wala kupewa misamaha.
Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema Dk Magufuli ameanza kazi vizuri kutokana na kuchukua hatua zinazolenga kuhakikisha Serikali inakuwa na fedha.
Alisema chama chake cha CCM kilitoa ahadi nyingi kwa wananchi wakati wa kampeni na hivyo ili kutimiza ahadi hizo ni lazima kodi zikusanywe na kubana matumizi ya Serikali.
Dk Benson Bana, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia alipongeza uamuzi wa kudhibiti walipa kodi akisema kama kila mmoja angekuwa analipa, nchi isingekuwa na utegemezi katika bajeti kama uliopo sasa.
“Wafanyabiashara wengi hawalipi kodi, wanashirikiana na wafanyakazi wenye dhamana ya kukusanya kodi kukwepa kodi, wanagawana fedha za Watanzania. Kama Rais Magufuli ameliona hilo, basi huo ni mwanzo mzuri,” alisema.
Dk Bana pia alisema Rais anatakiwa kuangalia eneo la matumizi ya magari kwa watumishi wa Serikali na kushauri walipwe posho ya mafuta badala kutumia magari ya kifahari ambayo alisema yanatafuna fedha nyingi za walipa kodi.
“Wanaotakiwa kutumia magari ya Serikali ni mawaziri na manaibu wao, makatibu wakuu, manaibu wao na wakurugenzi waandaliwe utaratibu mwingine wa kupewa posho ya usafiri ili watumie magari binafsi,” alisema.
Alisema hivi sasa inawezekana bosi akawa anaishi Bunju na dereva wake Mbagala ambako ndiko gari linakolala, hali ambayo alisema inasababisha kuwa na gharama kubwa za uendeshaji.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema iwapo Serikali ya Dk Magufuli itawategemea wafanyabiashara wadogo walipe kodi, haitaweza kutekeleza ahadi zake kwa sababu hakutakuwa na fedha.
Edward Porokwa, ambaye ni mkurugenzi wa shirika la PINGOs Forums, alisema kutaka walipakodi wakubwa walipe kodi, ni jambo zuri ambalo litaondoa misamaha ya kodi inayoliangamiza taifa.
Safari za nje hazina tija
Wachambuzi hao pia waliangalia agizo la kusitisha safari za nje hadi kwa kibali maalumu na kutaka shughuli ambazo zingefanywa na watendaji waliopo hapa nchini, zifanywe na mabalozi.
“Mabalozi sasa watakuwa na majukumu zaidi katika kuwakilisha nchi nje,” alisema Martine Masawe, mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye alimsifu Rais kwa uamuzi wa kusitisha safari za nje.
Alisema njia hiyo itapunguza matumizi makubwa ya nchi na kufanya fedha kuwa na matumizi katika masuala ya kusaidia vipaumbele vilivyopo.
Maoni hayo yanalingana na ya Dk Alexander Makulilo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)aliyesema safari za nje zimekuwa zikitumia fedha nyingi za walipakodi wakati kuna mabalozi wanaowakilisha nje ya nchi.
“Nashauri yeye ndiye awe mfano kwa kupunguza safari zake nje kwa sababu Rais na ujumbe wake hutumia gharama kubwa katika safari za nje,” alisema.
Lakini Dk Bana alikwenda mbali zaidi kwa kusema Rais anatakiwa kushikilia msimamo wake kwa kuwa suala la safari za nje limekuwapo tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza.
“Ikulu ndiyo ilikuwa inatoa vibali kwa watumishi wanaosafiri kwenda nje ya nchi, lakini usimamizi umekuwa mbaya na kusababisha watumishi kusafiri mara kwa mara nje ya nchi kwenye mikutano ambayo wakifika wala hawachangii chochote,” alisema Dk Bana ambaye amebobea kwenye sayansi ya siasa.
“Ameanza kazi vizuri kwa sababu eneo la safari za nje linapoteza fedha nyingi wakati watumishi wengi wanakwenda huko kwa ajili ya kufanya manunuzi.”
Pia Faraja Christotoms, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), alimtahadharisha kuwa maagizo hayo yasiwe nguvu ya soda.
“Kasi aliyoanza nayo siyo mbaya, tunaomba tu isiwe kama nguvu ya soda,” alisema.
“Hata Rais (wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete alianza hivyo hivyo kwa kutembelea wizara mbalimbali. Lakini hawa ni watu wawili tofauti. Tumpe muda tuone, labda ana dhamira nzuri na nchi yake.”
Hoja za wanaomkosoa
Maagizo na utendaji wa Rais katika siku zake nne za kwanza hayajakosa wakosoaji.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paul Losolutie alisema agizo la kutoa elimu bure linahitaji kwenda sambamba na vifaa vya elimu.
“Hata kama watasema elimu bure wakati bado shule hazina madawati na walimu hawalipwi vizuri itakuwa haina maana kusema elimu ni bure wakati wanafunzi katika fomu zao za kujiunga na shule wataambiwa waje na mchango wa maabara, madawati, mafyekeo, walinzi na majembe,” alisema.
Alishauri utekelezaji wake uwe ni pamoja na kufuta michango ya wazazi, akisema kwa sasa ada ya shule hizo ni Sh 20,000, lakini michango ya mwanafunzi anayeingia kidato cha kwanza inafikia Sh300,000 jambo ambalo ni mzigo kwa mzazi kuliko ada.
Mwanafunzi wa Chuo cha Mipango Dodoma, Godrick Ngoli, alisema uamuzi wa kutoa elimu bure ni mzuri, lakini ingefaa zaidi baraza la mawaziri kushirikishwa kwanza ili kupanga mipango ya utekelezaji wake kwa pamoja.
Mwingine aliyemkosoa ni Profesa Semboja ambaye alisema Dk Magufuli alitakiwa kwanza kuhakikisha mifumo yote ya Serikali inafanya kazi vizuri kwa namna inavyotakiwa.
Alisema iwapo Rais atafuatilia kila kitu, itafikia wakati atachoka na kuona mzigo mkubwa.
Alimshauri atumie siku 100 za kwanza kusoma mifumo inavyofanya kazi na kuwapa majukumu watendaji wake ili kurekebisha kasoro atakazokuwa amezibaini.
“Urais ni taasisi, na siyo kwamba Rais atafanya kila kitu mwenyewe. Rais Magufuli ahakikishe anakuwa na timu nzuri ya watendaji ambayo itamsaidia kusimamia yale yote anayotaka yafanyike bila yeye kusema neno,” alisema.
Pia, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Paul Rosolutie alitilia shaka utekelezaji wa elimu bure na kusema suala hilo linahitaji muda wa kutosha ili kuweka mipango ya utekelezaji wake bila kuathiri huduma nyingine muhimu kwa shule za umma.
“Hata zile Sh20,000 wanazolipa wanafunzi zilikuwa hazitoshi kutatua matatizo ya shule na Serikali inashindwa kupeleka fedha za wanafunzi. Sidhani kama hilo lilifanyika, vinginevyo itakuwa ni mzigo mkubwa kwa watendaji wa Serikali katika kulitekeleza,” alifafanua.
Wapinga kusitishwa safari
Marwa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe pia alipinga uamuzi wa kusitisha safari za nje akisema utasababisha matatizo kwa kuwa makubaliano mengi ya nchi huhusisha mawaziri na watumishi wa Serikali.
“Sasa kusema mabalozi ndiyo watakuwa wanawakilisha nchi katika baadhi ya mambo haitawezekana,” alisema.
Marwa alitoa mfano Rais aliyepita aliyesitisha safari zote za nje isipokuwa kwa kibali cha Serikali wakati akiingia madarakani mwaka 2005, lakini akakumbana na ugumu katika utekelezaji wa agizo hilo, na badala yake safari zikaongezeka.
Maoni ya wananchi
Wananchi wengine walioongea na Mwananchi pia walisifu hatua ambazo Dk Magufuli ameshachukua hadi sasa.
Mwenyekiti wa Kampuni za Ulinzi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kasimir Kubaja alisema kuzuia safari za viongozi nje ya nchi ni safi kwa sababu zinatumia fedha nyingi za kigeni wakati ukweli wapo mabalozi ambao wangeweza kutekeleza majukumu hayo.
Hata hivyo Kubeja alimshauri Rais Magufuli kufuatilia kwa ukaribu suala la wazabuni serikalini akisema fedha nyingi zinaibwa katika manunuzi.
Naye mhandisi wa umeme wa mjini Mbeya, George Mwang’ombe alisema kitendo cha kusitisha safari za nje kwa viongozi ni kizuri, lakini kiende sambamba na kupiga marufuku magari ya Serikali kwenda kwenye baa, kuzuia posho za vikao vya ndani na kuwabana watendaji wa halmashauri wafanye kazi za wananchi.
Mwang’ombe pia alishauri Serikali itoe fedha za uendeshaji kwenye shule za sekondari na za msingi ili kuepusha ukata utakaosababishwa na kutolewa elimu bure.
Mkurungezi wa asasi ya Kukuza Utawala na Uwazi Tanzania (IGT), Edwin Soko alisema Rais amefanya vizuri kufuta safari za nje na kwamba njia hiyo itamfanya aweze kutimiza ahadi zake, kama kutoa Sh50 milioni kwa kila Kijiji, kujenga barabra za kisasa pamoja na kununua meli mpya.
Ofisa Ustawi wa Jamii, Mwanza, Davis Justine alisema Dk Magufuli amefanya vizuri kuagiza wafanyabiashara wakubwa wabanwe na kulipaa kodi na kufuta safari za nje, kwa kuwa zilikuwa zinapoteza fedha nyingi ambazo zingewekezwa katika sehemu nyingine zingeleta maendeleo.
Sharon Sauwa, Lauden Mwambona, Lilian Lucas, Ngollo John, Peter Elias, Mussa Juma na Raymond Kaminyoge.
No comments:
Post a Comment