Hiace iliyopata ajali
***
WATU 12 wamekufa na wengine 22 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea kijiji
cha Ighuka wilayani Ikungi kwenye Barabara Kuu ya Singida – Manyoni
baada ya Toyota Hiace walimokuwa wakisafiria kutoka kumchukua bibi
harusi kugongana uso kwa uso na Toyota Noah iliyokuwa imepakia watu
kutoka msibani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba alisema kuwa ajali
hiyo ilitokea juzi saa mbili usiku kwa kulihusisha gari lenye namba za
usajili T 581 BBV iliyokuwa ikitokea Singida kwenda Manyoni na T 423 CFF
iliyokuwa ikitokea Manyoni kwenda Singida.
Alisema kuwa ingawa uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha ajali hiyo bado
unaendelea, taarifa za awali zinaonesha kuwa sababu kuu ni mwendo kasi
na uzembe wa madereva.
“Baadhi ya majeruhi walituambia dereva wa Toyota Hiace aliyekuwa anatoka
Singida mjini alihama kutoka upande wake na kwenda upande wa pili wa
barabara ambako aligongana uso kwa uso na Noah iliyokuwa imebeba watu
waliokuwa wakitoka msibani na kusababisha vifo vya abiria 10 hapo hapo
na majeruhi 24,” alisema.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa mkoa wa Singida, Dk Ng’hungu Kusenza
alisema kuwa majeruhi wawili waliofikishwa Hospitali ya Misheni Puma kwa
ajili ya matibabu pia walikufa hivyo kufanya idadi ya watu waliokufa
kuwa 12.
Aliwataja waliokufa ambao miili yao imehifadhiwa Hospitali ya mkoa kuwa
ni John Duma, Jasson Nsunza, Abubakar Omari, Mary Kinku, Mwanaidi Juma
na Husna Juma, Wengine ambao miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Misheni
Puma wilayani Ikungi ni Ezekiel Joseph, Mussa Daniel, Namtaki Daniel,
Hamis Omari, Jumanne Mganga na Wansola Shalua.
Habari ambazo hazijathibitishwa zinadai kuwa Bwanaharusi na madereva wa
magari yote mawili ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika ajali
hiyo.
No comments:
Post a Comment