
Mashabiki wa Ubelgiji na Manchester United jana walijawa na furaha baada ya kusikia kwamba mshambuliaji wao Romelu Lukaku amevunja rekodi ya ufungaji katika timu yao ya taifa.
Romelu Lukaku alitajwa kuvunja rekodi hiyo kwa kuwapita Bernard Voorhoof na Paul Van Himst ambao wana mabao 30 huku goli dhidi ya Japan likimfanya yeye kufikisha 31 idadi ambayo hata Lukaku mwenyewe alijinasibu kuifikia.
Lakini sasa shirikisho la soka duniani FIFA limeibuka na kutoitambua rekodi hiyo ya Romelu Lukaku kwa kusema kwamba moja kati ya michezo ambayo Lukaku alifunga hautambuliki na shirikisho hilo.
Mechi hiyo ilikuwa mwaka 2014 ambapo Ubelgiji walicheza dhidi ya timu ya taifa ya Luxembourg ambapo Ubelgiji waliibuka kidedea kwa mabao 5 huku Romelu Lukaku akifunga mabao 3 kati ya hayo 5.
Kinachowafanya FIFA kuundoa mchezo huo kwenye rekodi zao ni kitendo cha Ubelgiji kufanya sub 7 badala ya 6 katika mchezo huo suala ambalo lilikuwa kinyume na sheria katika mechi hiyo.
Hii sasa inamaanisha Lukaku ana mabao 28 tu na kama anahitaji kuwa mfungaji bora wa muda wote nchini Ubelgiji itambidi kufunga mabo matatu ili kufikisha 31.
No comments:
Post a Comment