MWENYEKITI WA BODI YA WAKURUGENZI TAWA AKAGUA NA KUZINDUA UJENZI WA MIUNDOMBINU KUPITIA MIRADI YA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19 KATIKA PORI LA AKIBA LA MKUNGUNERO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 22, 2022

MWENYEKITI WA BODI YA WAKURUGENZI TAWA AKAGUA NA KUZINDUA UJENZI WA MIUNDOMBINU KUPITIA MIRADI YA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19 KATIKA PORI LA AKIBA LA MKUNGUNERO



Na Mwandishi wetu 
Machi 21, 2022, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Meja Jenerali (Mstaafu), Hamisi Semfuko, amekagua na kuzindua ujenzi wa miradi mitatu (3) ya Miundombinu ya kuboresha Utalii katika Pori la Akiba la Mkungunero.

Tukio hilo lililofanyika Machi 21, 2022 limehusisha mradi wa ujenzi wa lango kuu la kuingilia wageni, ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 47.5 na ujenzi wa eneo la kupumzikia watalii 'Picnic Site' yote ikigharimu kiasi cha sh. Millioni 672.

Fedha hizo ni kutoka Mradi wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko- 19 na zinalenga kuboresha miundombinu ya Utalii katika Pori hilo la Akiba la Mkungunero, linalopatikana katika mikoa ya Dodoma na Manyara.

Akizungumza katika hotuba yake, Meja Jenerali (Mstaafu) Semfuko, ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha hizo na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuipatia TAWA kiasi cha sh. bilioni 12.9 kwa ajili ya kuboresha miundombonu ya Utalii.

Vilevile, Meja Jenerali (Mstaafu) Semfuko amesisitiza ufuatiliaji wa karibu wa miradi hiyo, ili kuhakikisha inajengwa kwa ubora uliokusudiwa kwa kuzingatia thamani ya fedha zilizotumika na kukamilika kwa muda uliopangwa.

Kadhalika, Mwenyekiti aliyeambatana na wajumbe wa bodi wa TAWA amewahakikishia wananchi wanaoishi pembeni ya Pori hilo la Mkungunero na maeneo mengine yanayosimamiwa na TAWA kuwa watanufaika na miradi hiyo.

Awali, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi (TAWA) Mabula Misungwi Nyanda, amesema miradi hiyo ni muhimu na itasaidia katika kuimarisha shughuli za Utalii na pia kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, mambo ambayo yatachangia kuongezeka kwa mapato ya serikali na wananchi.

Miradi mingine inayotekelezwa katika Pori la Akiba la Mkungunero ni ufungaji wa mfumo wa umeme jua, uchimbaji wa visima na ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 42 inayotekelezwa kwa fedha za Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

No comments:

Post a Comment