Na Mwandishi wetu, Mtwara
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo amefurahishwa kwa ushirikiano unaotolewa na viongozi wa mikoa ya Lindi na Mtwara katika kuhamasisha matumizi ya mbolea kwa wakulima wa maeneo hayo.
Alionesha kufurahishwa huko alipokutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Abdallah Malela tarehe 11 Machi, 2022 aliyeunga mkono juhudi za serikali katika kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia matumizi ya mbolea kwenye kilimo.
Katika kikao hicho, Dkt. Ngailo alikiri kupata ushirikiano kutoka mamlaka ya serikali za mtaa ikiwa ni pamoja na ofisi za Mkoa na Halmashauri husika katika kuhamasisha matumizi sahihi ya Mbolea na kuomba ushirikiano huo uendelee ili kufanikisha siku ya mkulima inayotarajiwa kufikiwa mapema mwezi Aprili 2022.
Alisema lengo la ziara yake katika mikoa hiyo ni kuwaelimisha wakulima na wananchi juu ya umuhimu wa kutumia mbolea na kubainisha kuwa kuna tofauti kubwa kati ya shamba lililopandwa na kukuzia kwa mbolea na lile ambalo halijatumia mbolea.
Aidha, aliziomba Serikali z a mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea kwenye kilimo ili kuwa na matokea chanya katika shughuli za kilimo.
Akiongea katika kikao kilichofanyika katika Ofisi yake Mkoani Mtwara, Katibu Tawala Malela alisema suala la kilimo ni agenda ya mkoa yenye lengo la kuwafanya wananchi wa Mtwara kupunguza utegemezi kwenye kilimo cha korosho pekee na badala yake wajihusishe na kilimo cha mazao mengine ya biashara na chakula.
Katika suala la uhamasishaji wa matumizi ya mbolea kwa wakulima, Mlale alisema watalifanya kwa uzito wake kwani ni sehemu ambayo wao kama mkoa wameamua kuifanyia kazi kikamilifu ili kuimarisha Sekta ya Kilimo katika Mkoa huo.
“Tunataka wakulima wasitegemee korosho tu wajihusishe na mazao mengine, tutafanya zaidi katika kuelimisha umma” alisisitiza Malela.
Aliendelea kusema, vipaumbele vya mkoa huo vimejikita katika mambo mawili muhimu ikiwa ni kilimo na elimu na baada ya uhamasishaji kwa wakulima kulima mazao yote huko mbele wataamua wenyewe kipi walime na kipi wasilime.
Aidha, aliwataka maafisa wa Mkoa waliohudhuria kikao hicho ikiwani pamoja na Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Amani Lusaki kuharakisha katika kusukuma masuala ya maendeleo mbele likiwemo la uhamasishaji matumizi ya mbolea.
“Kimbizeni hiyo ajenda kimbizeni iende, mtu akiona jambo dogo kwetu liwe kubwa, sisi hatuna viwanda hivyo tutajitangaza kwenye kilimo chetu na kila mwaka tutapandisha kipato kupitia kilimo” alikazia Malela.
Kauli mbiu ya siku ya mkulima kwa mwaka huu ni yenye kauli mbiu “Tumia mbolea kuongeza kipato na tija”.




No comments:
Post a Comment