WAZIRI AWESO: “SH.BILIONI 41 ZIMETOLEWA NA SERIKALI YA RAIS SAMIA KULIPA MADENI YA WAKANDARASI WA MIRADI YA MAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, March 11, 2022

WAZIRI AWESO: “SH.BILIONI 41 ZIMETOLEWA NA SERIKALI YA RAIS SAMIA KULIPA MADENI YA WAKANDARASI WA MIRADI YA MAJI


Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso

Na Mwandishi wetu, Dodoma 

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema kuwa serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi Bilion 41 ili kufanikisha watekelezaji wote wa miradi ya maji nchini Tanzania kulipwa madeni yao mara moja na kuwahakikishia upatikanaji wa uhakika wa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo.

Waziri Aweso ametoa kauli hiyo katika Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Maji Tanzania uliokutanisha Wakandarasi, Wahandisi Washauri, Wamiliki wa Viwanda, Wasambazaji wa Vifaa vya Ujenzi, Wasambazaji wa Dawa za Kutibu Maji, Kampuni za Utafiti na Uchimbaji Visima pamoja na Taasisi za Fedha uliofanyika Jijini Dodoma.

Akizungumza katika mkutano huo Waziri Aweso amesema kuwa Wizara ya Maji inathamini mchango mkubwa wa wadau na itahakikisha inalipa madai yote ya muda mrefu na kulipa kwa wakati madai yote yatakayoletwa na watoa huduma wote kwa kazi zinazoendelea.

Aweso amesema kwa kutambua hilo Wizara imechukua hatua za makusudi kuandaa mkutano huo kwa lengo la kusikiliza na kujadiliana kwa pamoja ili kupata suluhisho la changamoto zinazokwamisha ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maji.

Pia, amewashukuru wadau wote kwa mchango wao mkubwa katika mageuzi ya Sekta ya Maji na kusisitiza kuwa ufanisi wa Wizara unawategemea sana wao katika kutimiza dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani na kuendelea kuipaisha Tanzania kwenye uchumi wa kati.

Pamoja na kuwahakikishia ushirikiano wa dhati, hususani wale wote wenye uwezo na kufanya kazi kwa uaminifu, lakini akatoa onyo kwa wale wote wababaishaji kwa kusema kuwa hawatakuwa na nafasi pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafungia na hata kuwafutia kabisa usajili.

Aidha, Waziri Aweso amewaalika wadau wote wa Sekta ya Maji nchini katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani, tarehe 22 Machi, 2022 katika Ukumbi wa Mlimani City ambapo Mgeni Rasmi atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameomba wakandarasi kuwa waaminifu kwa kazi wanazopewa na Serikali, pamoja na kuwataka wale wachache wasio waaminifu kuacha tabia hiyo ili kuendelea kudumisha ushirikiano baina yao na Serikali kwa manufaa ya wananchi.

No comments:

Post a Comment