![]() |
| Kaimu Meneja wa TFRA kanda ya kaskazini akiingiza majina ya wakulima kwenye mfumo wa kidigitali wa ruzuku ili kuwawezesha kupata namba ya usajili na kununua mbolea kwa mfumo wa ruzuku |
Na Mwandishi wetu-Manyara
Mbolea ya ruzuku ni fursa iliyotolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tamzania kupitia Wizara ya Kilimo hivyo wakulima jitokezeni kusajiliwa ili muweze kunufaika na ruzuku hiyo ya mbolea.
Alisema, zoezi la kusajili wakulima linakwenda sambamba na kuwasilisha taarifa hizo za wakulima kwa Afisa Kilimo ili aweze kuzipandisha kwenye mfumo na kuwezesha mfumo wa manunuzi kuendelea kufanya kazi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria, wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Belinda Kyesi kwa nyakati tofauti alipotembelea vijiji vya Managhat, Himiti na Haraa wilayani Babati mkoani Manyara kwa lengo la kufuatilia mwenendo wa usajili wa wakulima mkoani Manyara.
Ukisajiliwa na huna pesa ya kununua mbolea hulazimishwi kununua mbolea ila usiposajiliwa hutaweza kununua mbolea maana mbolea zote zitauzwa kupitia mfumo wa ruzuku unaomtaka mkulima kujisajili.
Alisema serikali haijaweka kikomo cha kumsajili mkulima na kuwataka wajitokeze kujiandikisha kabla ya kuanza msimu wa kilimo ili taarifa zao zionekane kwenye mfumo na wawezeshwe kununua mbolea kupitia namba ya utambulisho watakayopewa.
Akizungumzia namna unavyofanyika usajili huo, Kaimu Meneja wa TFRA kanda ya Kaskazini, Gothard Liampawe alisema wakulima wanaanza kujisajili ngazi ya vijiji na kata na baadaye taarifa hizo zinaingizwa kwenye mfumo kupitia maafisa ugani wa maeneo yao.
Alisisitiza umuhimu wa kutekeleA jukumu hilo kwa wakati kila mmoja kwenye eneo lake ili kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa wakati bila mkwamo wowote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Managhat, Iddi Amma aliishukuru TFRA kwa kutembelea vijiji vyao kwani wamepata ufafanuzi wa masuala ya kusajili na kujulishwa kuwa zoezi hilo ni endelevu.
Aidha, Iddi alimtaka Bibi Shamba wa kijiji hicho, Happy Ernest kufanya kikao cha kuhamasisha wakulima kujisajili mara baada ya zoezi la sensa kukamilika ili wakulima wasipoteze fursa hii.
Alisema, walienda taratibu wakidhani tayari wamefikia kikomo cha kusajili lakini maadam zoezi hilo ni endelevu basi wataendelea kuhamasisha wakulima kujisajili ili kufikia lengo la serikali la kuwawezesha kupata mbolea kwa bei himilivu.





No comments:
Post a Comment