Nusu ya wananchi wanataja kupanda kwa gharama za maisha (48%) na kukosa fursa za kuzalisha kipato(29%).
Tarehe 25 Agosti 2022, Dar es Salaam: Matatizo makubwa matatu yaliyotajwa kuwasumbua zaidi wananchi kwenye kaya zao yote ni matatizo ya kiuchumi. Kati ya hayo, tatizo kubwa zaidi ni kupanda kwa bei za bidhaa na gharama za maisha (48%). Ikifuatiwa na ukosefu wa ajira na fursa nyingine za kuzalisha kipato (29%), vile vile matatizo ya njaa na uhaba wa chakula yanatajwa na wananchi wengi (26%). Mbali na matatizo ya kiuchumi wananchi wametaja matatizo mengine kwenye huduma za jamii: vituo vya afya (23%), upatikanaji wa maji safi (20%), huduma za usafiri (17%) na mapungufu katika sekta ya elimu (15%).
Twaweza imetoa matokeo haya kwenye jarida la utafiti lenye kichwa cha habari Hali ya Taifa - Uchumi: Uzoefu na maoni ya wananchi wa Tanzania kuhusu uchumi wa Taifa na tozo za miamala ya fedha kupitia simu.
Muhtasari huu unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za mkononi. Takwimu zilizowasilishwa zilikusanywa kutoka jopo maalumu la wahojiwa wa tafiti za awali zilizofanywa na Ipsos nchini Tanzania.
Wahojiwa walichaguliwa kinasibu, na jopo lilikuwa na uwakilishi wa kitaifa. Takwimu hizi ni za awamu ya saba ya utafiti kwa njia ya simu, ambapo jopo la wahojiwa 3,000 walipigiwa simu kati ya tarehe 18 Juni na 12 Julai
2022.
Walipoulizwa ni jambo gani ambalo wangependa Rais kulishughulikia kama suala la kipaumbele, wananchi walitaja kupanda kwa gharama za maisha (46%) na hali ya vituo vya afya (42%). Eneo la tatu linalotajwa na wengi kama kipaumbele cha kushughulikiwa na Rais ni huduma za usafiri (35%). Pia wananchi wanataka serikali zao za mitaa ziboreshe utoaji wa huduma za jamii, hasa huduma za usafiri (44%), vituo vya afya (35%) na upatikanaji wa maji safi (26%) kama vipaumbele vyao vikuu.
Licha ya matatizo yaliyotajwa, wananchi wengi wanasema wameona kuboreshwa kwa huduma za jamii katika kipindi cha miezi sita iliyopita, hasa sekta ya elimu (68%). Wengi pia wanasema uhuru wa kujieleza umeboreshwa (60%), uhuru wa kisiasa umeimarika (56%), ulinzi na usalama (59%) na kupungua kwa unyanyasaji dhidi ya wanawake (61%) na watoto (60%). Hata hivyo, idadi kubwa ya wananchi (68%) wanasema gharama za maisha zimepanda zaidi katika kipindi hicho, na wananchi wanasema upatikanaji wa ajira na fursa za kujipatia riziki za maisha vimepungua (48%) badala ya kuongezeka (22%).
Kwa ujumla, wananchi wengi wanasema nchi iko kwenye mwelekeo sahihi (30%) wachache wanasema nchi haiko kwenye mwelekeo sahihi (25%), ingawa wengi zaidi (44%) wana halil ya sintofahamu kuhusu mwelekeo wa nchi. Matumaini ya wananchi kuhusu suala la uchumi yako chini sana. Idadi ya wanaosema hali ya uchumi ni mbaya ni mara nne (41%) ya wale wanaosema uchumi ni mzuri (9%).Idadi kubwa ya wananchi wametumia huduma za fedha kupitia simu za mkononi mwezi uliopita (75%).
Karibu nusu yao (47%) walitumia huduma hizo wiki iliyopita. Wakazi wa Dar es Salaam wanaitumia zaidi huduma hiyo (80%), wakifuatiwa na kundi la vijana wenye umri wa miaka 30-39 (77%). Wananchi wenye elimu ya sekondari na zaidi (92%) na wananchi walio kwenye ajira rasmi (89%) ni watimuaji wakubwa wa huduma za fedha kupitia
simu za mkononi
Wananchi nane kati ya kumi (80%) wanafahamu kuhusu tozo mpya ya miamala ya fedha kwa njia ya simu,wakati zaidi ya nusu ya wananchi (55%) wanafahamu kuhusu kupunguzwa kwa tozo hizo kulikopitishwa mwezi Novemba 2021. Mwezi huo huo Novemba, mwananchi 1 kati ya 3 (34%) hakuunga mkono kuanzishwa kwa tozo hizo, wakati mwezi Julai 2022 idadi sawa na hiyo (28%) hawakukubaliani wala kuunga mkono punguzo la tozo
hizo.
Karibu mara tatu ya wananchi (44%) waliripoti kuwa wamepunguza kutuma fedha kwa njia ya simu. Na kiasicha fedha wanachopokea kupitia simu kimepungua tangu mwezi Julai 2021, tofuati na wachache (15%) walioongeza idadi ya miamala katika kipindi hicho.
Maoni ya wananchi kuhusu tozo za miamala ya fedha kwa njia ya simu yanatofautiana. Wananchi wengi wanakubali kuwa tozo hiyo ni njia muhimu ya serikali kukusanya mapato (67%), na kwamba inasaidia kumfanya kila mtu achangie maendeleo ya taifa (63%). Lakini wachache wanakubali kuwa tozo hiyo itapunguza utegemezi kwa wafadhili (46%), au wanakubali tozo za miamala ya fedha kwa njia ya simu ni kitu zuri (43%).
Wananchi wanaonesha dalili kuwa wangeunga mkono zaidi tozo hizo iwapo wangekuwa na taarifa kamili kuhusu matumizi ya fedha zinazokusanywa kupitia tozo. Wengi (63%) wanasema wangekuwa tayari zaidi kulipa tozo iwapo wangeweza kufuatilia matumizi ya fedha hizo. Wachache (39%) wanasema wanajua pesa zinatumikaje au wanaweza kutafuta kwa urahisi taarifa kutoka serikalini juu ya matumizi ya mapato ya tozo (44%).
Wananchi wanataja miradi mbalimbali ambayo wangependa yanufaike na tozo za miamala. Eneo la kwanza kabisa ni huduma za afya (57%) na elimu (50%), ikifuatiwa na ujenzi wa barabara (38%), huduma za maji (33%),umeme (20%), kilimo (18%) na mikopo (17%). Pia wamependekeza maeneo mengine mengi.
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, alisema, "Maoni ya wananchi kuhusu tozo za miamala ya fedha kwa njia ya simu yanadhihirisha changamoto ya utawala. Serikali haina budi kupanua wigo wa kodi ili kuongeza mapato yatakayo gharamia huduma za jamii. Kupanua wigo wa walipakodi kunawashirikisha wananchi wengi zaidi kwenye mipango ya maedeleo na kuwafanya wadai uwajibikaji kwa serikali.
"Lakini huduma za fedha kwa njia ya simu zimesaidia sana kwenye biashara na mapato ya familia. Tozo zimepandisha gharama za huduma hizi muhimu, zimewafanya wananchi wapunguze kwa kiasi kikubwa matumizi ya huduma hizi na huenda zikaathiri ukusanyaji wa mapato,” aliendelea.
“Je, Serikali inapaswa kufanya nini kusawazisha mambo haya mawili yanayokinzana ili kujenga jamii yenye haki? Jibu mojawapo ni kuzisikiliza sauti za wananchi inapofanya maamuzi makubwa kama haya ya tozo.Usikivu wa serikali utasaidia kujenga imani ya wananchi, na kuiongeza ari yao ya kuchangia maendeleo kwa hali na mali.” alihitimisha.


No comments:
Post a Comment