Nchi 5 za Afrika zaweka mkakati wa kutoa mafunzo na kuajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, March 8, 2023

Nchi 5 za Afrika zaweka mkakati wa kutoa mafunzo na kuajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii


Na. WAF-Rwanda

Mawaziri wa Afya wa nchi 5 ikiwemo Tanzania, Rwanda, Sierra Leon, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekutana na kuweka mkakati wa kutoa mafunzo rasmi angalau ya mwaka mmoja, hatimaye kuajiri Wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa ajili ya kuimarisha Huduma za Afya ya Msingi.

Haya yamejadiliwa jana kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Mawaziri wa Afya wa Afrika unaofanyika Jijini Kigali-Rwanda, ambapo wanajadili mifumo endelevu na stahimilivu ya uimarishaji wa huduma za afya ikiwemo masuala ya kuwatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii. Mkutano huu umeandaliwa na Taasisi ya Susan Thompson Buffet Foundation (STBF).

Wahudumu hao watatekeleza afua jumuishi ngazi ya jamii ikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto, afua za lishe na afua za tahadhari na kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko. Vilevile nchi wanufaika zitatumia mifumo ya ulipaji fedha Serikalini katika utekelezaji wa mpango huo sambamba na kuweka utaratibu wa kuwawezesha Wahudumu hawa kujiendeleza kitaaluma (career development systems).


Akizingumza katika Mkutano huo Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali ya Tanzania tayari inayo Muundo wa Utumishi (Scheme of Service) unaoitambua kada hiyo katika kutekeleza majukumu yao kama Wasaidizi wa Afya (Health Assistants) ngazi ya vituo vya kutolea huduma za afya na katika ngazi ya jamii

Tanzania ina uzoefu wa kuendesha mafunzo ya mwaka mmoja kwa kada rasmi ya wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ambapo zaidi ya Wahudumu 9,800 walihitimu mafunzo hayo kwa mwaka 2017 hadi 2019.

Waziri Ummy ameongeza kuwa Wizara yake itajikita katika kutekeleza Mpango huo kwa kuwajengea uwezo na kuwaajiri Wahudumu 15,000 kwa kipindi cha miaka mitatu yaani mwaka 2023/24 hadi 2025/26 ambapo kwa kuanzia Wahudumu wapatao 5,000 watapewa mafunzo kupitia Vyuo vya Afya vya kati kwa mwaka wa fedha 2023/24. 


Wahudumu hawa watatekeleza afua jumuishi ikiwemo Afya ya Mama na Mtoto, Lishe, Magonjwa Yasiyoambukiza, Magonjwa ya Mlipuko na Magonjwa Yanayoambukiza (VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria), Amesema Waziri Ummy.

Naye Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Nassor Mazrui, amesema Wizara yake inatarajia kuwatumia Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii katika utekelezaji wa huduma za kipaumbele ikiwemo Magonjwa Yasiyoambukiza, Magonjwa ya Mlipuko na Afya ya Mama na Mtoto kwa ngazi ya Shehia zote visiwani Zanzibar. 

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Susan Thompson Buffet Foundation, Prof. Senait Fisseha amesema kuwa Taasisi yake inalenga kushirikiana na nchi wanufaika katika utekelezaji wa Mpango Endelevu na Stahimilivu wa Kuwatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, lengo kuu ni kuboresha afya ya mama na mtoto sambamba na kuimarisha afua jumuishi za afya ngazi ya jamii. 

Naye Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Matshidiso Moeti amesisitiza kuwa ni muhimu kuimarisha mifumo ya TEHAMA ya utoaji wa taarifa na kuhakikisha kuwa Mipango ya kuwatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii inakuwa jumuishi kwa afua mbalimbali za vipaumbele katika nchi husika kwa kuendeleza ushirikiana na Wadau mbalimbali kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali. 

Mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Nchi na Serikali barani Afrika uliofanyika mwezi Julai, 2017 ambapo iliazimiwa kuwa jitihada za dhati zichukuliwe katika kutoa mafunzo na kuajiri angalau Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wapatao 2,000,000 ili kukidhi mahitaji ya huduma za afya ya jamii kwa kuzingatia ongezeko la sasa la watu barani Afrika.
 




No comments:

Post a Comment