Serikali imesema mmomonyoko wa Maadili ni kikwazo kikubwa kwa Maendeleo ya Taifa na sababu ya Wananchi kutofikia malengo yao.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum,Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa Mafunzo kuhusu masuala ya Maendeleo ya Jamii kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii yaliyoandaliwa na Wizara hiyo, jijini Dodoma Mei 10, 2023.
“Sekta zote muhimu za Maendeleo hutegemea Jamii yenye Maadili ili kuweza kuyafanikisha yote hayo”Alisema Dkt Gwajima.
Aidha, Dkt. Gwajima ameeleza umuhimu wa Taasisi na Vyuo vinavyotoa Mafunzo ya Maendeleo ya jamii na Mchango wake katika Taifa.
“Mustakabali wa nchi unategemea Taasisi na Vyuo mbalimbali kutoa Mafunzo na kuandaa Wataalam ambao watakuja na Masuluhisho ya Kisayansi na kutoa ushauri elekezi kwa ajili ya kukabiliana na kutatua Changamoto mbalimbali katika Jamii.”Amesema Dkt Gwajima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya jamii Fatma Toufiq amesema Mafunzo hayo yatawasaidia katika kuishauri Serikali.
“Mawasilisho haya yatatusaidia kuishauri Serikali hususani utekelezaji wa majukumu ya Wizara hii changa katika bajeti inayokuja ili Wizara hii iweze kuangaliwa kwa jicho la tofauti na kupewa kipaumbele kwani ni Wizara inayoilenga Jamii moja kwa moja”Amesema Toufiq.
Akieleza lengo la mafunzo hayo,Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum,Patrick Golwike amesema kupungua au kumalizika kwa Ukatili katika jamii ni kiashiria chema kwa Jamii hiyo kuendelea.
“Ukitaka Mabadiliko lazima mtaalam wa Maendeleo ya Jamii awepo kwani yeye ndiye anaunganisha wataalam wa kada mbalimbali kwa kuwa kazi yake kubwa ni kutengeneza tabia fulani kwa watu ili wataalam wa kada nyinginezo waweze kufanya kazi inayotakiwa”Amesema Golwike.
No comments:
Post a Comment