Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amewataka Wachimbaji Wadogo kupitia Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) kushirikiana na Wizara hiyo katika shughuli za uchimbaji ili kuweza kuinua sekta ya uchimbaji mdogo nchini.
Amesema ushirikiano mzuri baina ya wachimbaji na Wizara utaiwezesha Sekta ya Madini kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
Aidha, Mahimbali amesema wakati Wizara inajizatiti kuweka na kusimamia Mikakati na Sera zenye nguvu ili kuimarisha sekta ya uchimbaji mdogo ni wajibu wa wachimbaji kuchimba kwa weledi ili kuongeza mapato na kulipa kodi na maduhuli.
Amewataka kuwa wawazi katika kutatua kero na changamoto ili kuiwezesha Serikali kuondoa vikwazo katika uchimbaji kwa urahisi na kuahidi kuendelea kutatua changamoto zinazowasilishwa Wizarani kwa uharaka.
Naye, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga amewataka wachimbaji wa madini kutambua namna Wizara inavyowathamini na kufungua milango ili kuweza kutatua kero na kuleta maendeleo kupitia sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo ni mlezi wa wachimbaji wadogo, amesema FEMATA inapaswa kujua kwamba Serikali ina msukumo mkubwa katika kuwasaidia wachimbaji wadogo ni wajibu wao kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa Wizara.
Amepongeza jitihada za Shirikisho hilo kwa kuonesha nia ya dhati ya kutaka kuendelea na kukuza uchumi wa Serikali kupitia sekta ya wachimbaji wadogo ambao wengi wao ni wazawa.
Amesema Sekta ya Madini inawagusa watanzania na kwamba kuendeleza wachimbaji wadogo ni kuendeleza maisha ya watanzania wanaotegemea sekta hiyo.
Akitoa shukrani kwa Wizara, Makamu Mwenyekiti wa FEMATA Alfred Luvanda amesema hafla hiyo imekuwa na tija sana katika sekta ya wachimbaji wadogo.
"Ni nafasi adhimu kuona watendaji wakuu wa Wizara wanatenga muda kukutana na wachimbaji moja kwa moja, hali hii inaamsha imani ya wachimbaji kwa Serikali," amesema Luvanda.
Ameiomba Wizara isaidie kuwaunganisha wachimbaji wadogo wote ili waweze kufanya kazi chini ya mwamvuli moja ili kuimarisha sekta hiyo.
Ameipongeza STAMICO kwa kuendelea kuwasimamia vizuri wachimbaji wadogo licha ya majukumu makubwa waliyonayo.
No comments:
Post a Comment