Mwenyekiri wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania Dkt. Anthony Diallo amesema kuwa dhana iliyojengeka kwa watu wengi kuwa mbolea hususan za viwandani zinaharibu udongo ni potofu.
Dkt Diallo ameyasema hayo jana katika kikao kazi kati ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella na watendaji wake, Bodi ya Wakurugenzi wa TFRA, vyama Vikuu vya Ushirika na wataalamu wa kilimo mkoani humo.
Dkt. Diallo amesema kuwa utumiaji wa mbolea za viwandani kwa usahihi unaongeza uzalishaji na tija shambani na wala sio kuchakaza ardhi na hivyo kumsaidia mkulima kujikwamua kiuchumi.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa watu wengi wasiotaka kutumia mbolea husingizia kuwa mbolea inaharibu udongo hivyo Mamlaka itaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea nchini na amewataka wakulima kuondokana na dhana hiyo potofu.
Akizungumza awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella amesema tayari Mkoa wake umeshafanya maandalizi ya msimu wa kilimo kwa mwaka 2023/2024 na amemshukuru Rais Samia kutoa tena ruzuku kwa wakulima.
Mhe.Shigella amesema kuwa mkoa wake tayari umewahamasisha wakulima kununua mbolea mapema na kuainisha maghala katika kila kata yatakayotumika kuhifadhia mbolea hizo na hivyo ameitaka TFRA kuyaelekeza makampuni kufikisha pembejeo hiyo muhimu kwa wakati.
Lengo ya ziara ya Bodi ya Wakurugenzi wa TFRA katika Kanda ya Ziwa ni kujitambulisha kwa wadau na kusikiliza changamoto zinazowakabili ili kutoa ufumbuzi na kuelezea mikakati ya serikali ya usambazaji wa mbolea katika msimu wa kilimo 2023/2024.
No comments:
Post a Comment