Na Mwandishi wetu Kigoma
Uwekezaji katika uboreshaji wa miundombinu mbalimbali katika bandari za ziwa Tanganyika umeonmgeza ufanisi wa bandari hizo na kuziwezesha kuhudumia tani 294,731 kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Julai,2022 mpaka Juni,2023.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano wa kwanza wa Kamati ya Maboresho ya Huduma za Bandari kwa bandari za ziwa Tanganyika uliofanyika katika ukumbi wa Bandari ya Kigoma mkoani humo kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Huduma za Usafiri kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi-Sekta ya Uchukuzi Mhandisi Aron Kisaka amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa Shilingi Billioni 100 kwa ajili ya kufanya maboresho makubwa kwenye Bandari 9 kati ya 19 za Ziwa Tanganyika ikiwemo kuongeza magati ,kujenga maghala ya kuhifadhia mizigo , majengo ya abiria , utawala na kujenga bandari kavu ya Katoshi ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji katika ziwa Tanganyika.
Mha Kisaka amesema kutokana na uwekezaji huo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 Bandari za ziwa Tanganyika zimeweza kuhudumia jumla ya tani 294,731 ambapo tani 283,919 ni za mizigo inayoelekea nje ya nchi hususani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, tani 10,813 mizigo ya ndani ya Nchi, makasha 370 na abiria 186,746 wamehudumiwa
“Maboresho yaliyofanyika katika bandari hizi yamechangia sana kuongeza uhudumiaji wa shehena za mizigo na abiria kwa kuwepo miundombinu rafiki inayorahisisha ufanyaji biashara katika ziwa hili na sasa mizigo inapakiwa na kupakuliwa melini kati ya siku moja mpaka mbili hivyo kuvutia watumiaji zaidi” amesisitiza Mhandisi Kisaka
Kwa upande wake Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Bw. Edward Mabula amesema katika kuboresha huduma za bandari hizo Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeshaingia makubaliano na Serikali ya Kongo DRC kwa ajili ya kujenga bandari kavu eneo la Kalemi na Kasumbalesa na tayari Serikali ya kongo imeshatoa eneo kinachoendelea sasa ni kufanya tathmini ili kupata haki za umiliki ili ujenzi uanze mara moja na hii itaboresha ufanyaji kazi wa bandari za Ziwa Tanganyika kwa kuongeza shehena zaidi za kusafirisha nje ya Nchi.
“Makubaliano haya yatachochea biashara baina ya Nchi hizi mbili na hii ni fursa kwa bandari zetu kuhudumia shehena zaidi na kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 Bandari za Ziwa Tanganyika tumepanga kuhudumia shehena zaidi ya Tani 330,000 na kukusanya Billioni 11 na Meli mpya nne za Mizigo, Abiria na chelezo vinatarajiwa kujengwa” amesisitiza Mabula
Naye Mdau wa Bandari nchini na Mkurugenzi Mtendaji wa Malagarasi Shipping Company Bw Mbarak Hamoud ameishukuru Serikali na Wizara Sekta ya uchukuzi kwa kuanzisha vikao vya kamati za maboresho ya bandari kwa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma na sasa changamoto zao za uwekezaji zitatatuliwa kupitia vikao kwani kampuni yake toka Novemba,2022 imeanza ujenzi wa Meli mpya ya Mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 1,200 itakayofanya kazi kwenye bandari zote za Ziwa Tanganyika na Nchi Jirani na ujenzi wake umefikia asilimia 50 ambapo inatarajiwa kukamilika March,2024
Ziwa Tanganyika lipo katika Mikoa mitatu ya Kigoma, Katavi na Rukwa huku kukiwa na Bndari 19 katika mikoa hiyo na Wilaya za Kigoma, Kibirizi, Ujiji, Kagunga, Lagosa, Sibwesa, Ilagala, Sinuka, Sigunga, Lukoma, Karema, Ikola, Kasanga, Kabwe, Kipili, Kirando, Msamba, Mpasa na Wampembe ambapo jumla ya Meli na Boti ndogondogo zilizosajiliwa na zinazotoa huduma katika Bandari hizo ni 532
No comments:
Post a Comment