Angela Msimbira OR- TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Angellah Kairuki amewataka Maofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri 51 zilizopata magari mapya kuyatumia vizuri ili kuongeza ufanisi na ubora wa elimu kwenye maeneo yao.
Akizungumza Julai 5, 2023 jijini Dodoma kwenye hafla ya kukabidhi magari hayo, Kairuki amesema magari hayo yatumike kutembelea na kukagua shule, kufuatilia maendeleo ya ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kushughulikia kero za walimu ili kuleta ufanisi.
“Tunaamini kwamba hakutakuwa na visingizio kwa ninyi kutembelea na kukagua shule pia kashughulikieni kero za walimu huko shuleni kwao badala ya kuwasubiri wawafuate ofisini,”amesema Kairuki
Aidha, ametoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia matumizi sahihi ya magari hayo na kutenga bajeti za matengenezo.
" Serikali inafanya haya yote ili kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 Sura ya Tatu Ibara ya 78 inayoelezea Sekta ya Huduma ya Jamii kwa upande wa Elimu," amesema
Amewakumbusha Maofisa hao kusimamia kwa karibu ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari unaoendelea kujengwa nchi nzima hasa ya Kidato cha Tano ili wanafunzi wanaporipoti tarehe 13 Agosti, 2023 wakute mazingira rafiki ya kujifunza.
Naye, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Dkt. Charles Msonde, amesema kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Sekta ya Elimu (EP4R) hadi sasa magari 146 yamegaiwa ili kusaidia Maofisa hao shughuli za kielimu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Dennis Londo, amesema magari hayo ni nyenzo muhimu na ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya kuweka mazingira rafiki kwa watumishi wa elimu.
No comments:
Post a Comment