Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amoni Mpanju, amewataka wadau wa kampeni ya Serikali ya Linda Maadili, Wizara za kisekta, Wazazi, walezi na Jamii kwa Ujumla kuja na mbinu zitakazozuia watoto kupandikizwa mafundisho potofu.
Wakili Mpanju amesema hayo katika kikao cha wadau wanaosimamia Maadili kwa watoto na Jamii kukabiliana na mmomonyoko wa Maadili nchini kwa kuwakutanisha Watalamu kutoka Wizara za kisekta na Taasisi mbalimbali kilichofanyika Jijini Dodoma Julai 5, 2023.
Amesema mafundisho potofu ambayo hupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii yana athari kubwa kwa watoto na jamii na kuongeza kuwa iwapo hayatadhibitiwa, Athari zake zake zitakuja kuiumiza jamii siku za usoni.
"Haya tunayoyaona leo ya wanadamu wenzetu kujiita Mungu wala hayakuibuka tu ni kwa sababu ya mafundisho potofu yaliyopandwa ndani yao, Sisi kama Wizara yenye Dhamana ya watoto na jamii pamoja na juhudi Serikali inazozichukua kupitia Wizara za kisekta tukaona ni lazima tukutane sababu hili linagusa watoto na kesho ya nchi hii tujadiliane, mje na utaalam wenu tuje na suluhu ya kudumu ya nini hasa tukifanye ili lengo la kuilinda jamii ya kitanzania" amesema Wakili Mpanju
Wakili Mpanju ameongeza kuwa kila mwanajamii, Mzazi na mlezi analo jukumu la kuhakikisha anamlinda mtoto na kuzingatia Maadili.
Awali akiwasilisha hatua ambazo kamati hiyo kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wamefanya katika kampeni ya Linda Maadili Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Linda Maadili Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao amesema wamekua wakitumia kila nafasi kuhimiza suala la kulinda Maadili
"Kila taasisi kwetu tumeona ni fursa kuitumia kufikisha ujumbe na kuigusa jamii, Lengo letu ni kuangalia watoto wetu wanapata Maadili mema kwa kupitia nyanja mbalimbali na fursa mbalimbali zilizopo lakini kwenye njia ambazo zipo hatuanzishi vitu vipya kwa sababu tunajua Makanisa yapo, wanajamii na Viongozi wa dini wapo tunachofanya ni kwenda kuhamasisha na kupeleka zile jumbe ambazo sisi tunatamani zisambae" amesema Mayao
Kwa Upande wake Muwakilishi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Emmanuel Urassa amesema Tayari wameanza tafiti kuangalia nchi nyingine zinavyo kabiliana na changamoto hii na kuona ni namna gani wanaweza kuja na sera ya ulinzi wa mtoto mtandaoni ambayo itakidhi mahitaji ya muktadha wa sasa na baadae.
"Sisi tumeshaanza kuandaa Online Child protection ambapo pia tumeshafanya tafiti katika mataifa mengine kuona jinsi wao wanafanya kulinda haki za watoto na maudhui yasiofaa, ili tutoke na sera moja, na tutahakikisha wale wale wote ambao wamekuwa wakizalisha maudhui ya mtandao watatakiwa waweze kufuata sera za Nchi yetu " amesema Mhandisi Urassa
Naye Muwakilishi kutoka Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Yuda Semi amewasihi Maafisa Utamaduni kote Nchini wawapo katika shughuli za kitamaduni zinazokutanisha idadi kubwa ya watu kuhakikisha wanapenyeza ajenda ya kulinda maadili huku Muwakilishi kutoka Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Yusuph Ndosi akisema Baraza hilo tayari limeshakamilisha muongozo Maadili ambao utakwenda kugusa maeneo yote wanayoyasimamia ili kuleta tija kwa jamii hususani watoto.
No comments:
Post a Comment