VETA YAANDAA KONGAMANO LA UJUZI NA AJIRA,KUFANYIKA DODOMA AGOSTI 24,2023 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, August 22, 2023

VETA YAANDAA KONGAMANO LA UJUZI NA AJIRA,KUFANYIKA DODOMA AGOSTI 24,2023


Na Okuly Julius-Dodoma

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) kupitia programu yake ya Kukuza Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo Afrika (E4D), imeandaa Kongamano la Ajira (Job and Skills Fair) litakalofanyika Siku ya Alhamisi, tarehe 24 Agosti, 2023, katika Uwanja wa Nyerere Square jijini Dodoma kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 22,2023 Jijini Dodoma kuelekea kongamano hilo ,Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu -VETA ,Abdallah Ngodu amesma hadi sasa jumla ya vijana 3,258 wamenufaika na mafunzo katika vyuo vya VETA vya Dodoma, Manyara, Lindi, Singida, Mikumi, Gorowa na Dakawa katika awamu nne (4) huku udahili wa awamu ya tano ukiendelea na mafunzo hayo yametolewa kwa wiki nane (8) vyuoni na wiki nane (8) mahali pa kazi.



"Wakati wa kongamano hilo kutakuwa na maonesho ambayo yamelenga kujenga uelewa juu ya fursa za ufundi stadi zilizopo kwenye Mradi, kukuza uwezo wa kuajirika (Kujiajiri/Kuajirika) kwa wahitimu/wanufaika wa kozi zinazotolewa na Vyuo vya VETA chini ya Mradi wa E4DT, Vilvile kupitia Kongamano hilo wanafunzi/wanufaika watakutanishwa na waajiri ili waweze kushirikishana kuhusu taarifa za soko la ajira. Halikadhalika Wahitimu wataonesha umahiri wa ujuzi wao katika bidhaa walizotengeneza na miradi yao wanayotekeleza,"


Na kuongeza kuwa "kupitia kongamano hili wananchi watapata fursa ya kujionea shughuli zinazofanywa na wahitimu/wanufaika wa mradi wa E4DT pamoja na kupata taarifa juu ya fursa za mafunzo ya ufundi stadi zinazopatikana kwenye vyuo vya VETA nchini,"ameeleza Ngodu



Ngodu amebainisha kuwa utekelezaji wa Mradi wa E4D unahusisha ushiriki wa viwanda ambapo mpaka sasa viwanda/makampuni zaidi ya 20 yamethibitisha kushiriki na kuonesha huduma na bidhaa zao kupitia kongamano hilo.


"Tunaamini kuwa makampuni pia yatapata fursa muhimu ya kuthibitishiwa kwa uhalisia kuhusu umahiri na ujuzi wa wahitimu/wanufaika wa mafunzo ya ufundi stadi ili wajenge imani na hatimaye kuwapatia fursa za ajira vijana hao," amesema Ngodu



Amesema kuwa wakati wa Kongamano hilo, kutakuwa na uwepo wa Taasisi za Fedha ambazo zitatoa fursa za uwezeshwaji hususan mikopo zinazoweza kuwanufaisha vijana waliopata ujuzi ili wawe na mitaji ya kuendesha shughuli za uzalishaji na kuongeza vipato na ajira endelevu


Tanzania ni miongoni mwa nchi sita za Afrika zinazotekeleza mradi wa Stadi za Ajira kwa Maendeleo Afrika (E4D) unaofadhiliwa na Wizara ya Shirikisho la Ujerumani la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ) na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Korea (KOICA). Mradi wa E4DT ulianza kutekelezwa mwezi Mei, 2022, ukilenga kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa vijana 4000 nchini, katika fani za Ufundi Bomba wa majumbani (Domestic Plumbing), Ufundi Bomba Viwandani (Industrial Plumbing), Ufundi wa Uchomeleaji Vyuma Viwandani (Industrial Welding) na Ufundi wa Mekatroniki (Mechatronic). Hadi sasa jumla ya vijana 3,258 wamenufaika na mafunzo katika vyuo vya VETA vya Dodoma, Manyara, Lindi, Singida, Mikumi, Gorowa na Dakawa katika awamu nne (4). Udahili wa awamu ya tano ukiendelea na mafunzo hayo yametolewa kwa wiki nane (8) vyuoni na wiki nane (8) mahali pa kazi.


Kongamano Hilo linabebwa na Kauli mbiu isemayo “Ufundi Stadi kwa Fursa zaidi za Ajira”

No comments:

Post a Comment