TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA WAZIRI BASHUNGWA LA KUPANDA MITI MAENEO YA BARABARANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, January 30, 2024

TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA WAZIRI BASHUNGWA LA KUPANDA MITI MAENEO YA BARABARANI

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Zuhura Amani, akiongoza zoezi la kupanda miti ya kivuli katika barabara ya Chimwaga – St. Peter Claver ikiwa ni moja ya maelekezo ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, leo Januari 30, 2024 jijini Dodoma.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Zuhura Amani, akimwagili maji miti ya kivuli katika barabara ya Chimwaga – St. Peter Claver ikiwa ni moja ya maelekezo ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, leo Januari 30, 2024 jijini Dodoma.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Zuhura Amani, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), katika zoezi la upandaji miti ya kivuli katika barabara ya Chimwaga – St. Peter Claver ikiwa ni moja ya maelekezo ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, jijini Dodoma.
Baadhi ya Watumishi wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma wakipanda miti ya kivuli katika barabara ya Chimwaga – St. Peter Claver ikiwa ni moja ya maelekezo ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, jijini Dodoma.

Na Okuly Julius-Dodoma 

Wakala wa Barabara (TANROADS) Jijini Dodoma imeanza kutekeleza agizo lililotolewa jana January 29,2024 na Waziri wa Ujenzi Mhe.Innocent Bashungwa la kupanda miti maeneo ya barabara kwa ajili ya kuendelea kupendezesha miji nchini na kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Meneja Ofisi ya Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Zuhura Amani amesema kuwa
Ofisi yake inaendelea kutekeleza maelekezo ya viongozi ya kupendezesha mji wa Dodoma na pia imeweka utaratibu wa kuendelea na zoezi hilo Katika Barabara zake zote.

Mhandisi Zuhura amesema Leo Januari 30, 2024 Jijini Dodoma, mara Baada ya Kumaliza zoezi la upandaji miti na kusisitiza kuwa jumla ya miti waliyoipanda toka mwaka juzi 2022 ni takribani 2089, na mwaka huu wa fedha wamepanga kuendelea na zoezi hilo ambapo watapanda miti 540 ndani ya jiji Hilo.

"Leo hii tunatarajia kupanda miti takribani 114 ambayo tumeiandaa na wafanyakazi wote wa TANROADS wamejipanga na tupo tayari kufanya zoezi hili", Amesema Mhandisi Amani

Amesema miti hiyo waliyoipanda wataendelea kuitunza kwa kuhakikisha kwamba inakua na inafikia malengo ambayo wamejiwekea, na kusisitiza Kuwa ingawa kuna changamoto ya hali ya hewa lakini watahakikisha wanaendelea kuitunza miti kwa kuimwagilia maji wakati wa kipindi cha kiangazi.

"Mkoa wetu wa Dodoma una kipindi kirefu sana cha kiangazi lakini TANROADS tutahakikisha tunaendelea kuitunza na kuiwekea mbolea ili iweze kustawi zaidi" alisema.

Kwa upande wake Mfanyakazi wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Elisony Mweladzi amesema amehamasika kutokana na zoezi hilo la upandaji miti, hivyo yeye pamoja na wafanyakazi wengine wataendelea kutekeleza maelekezo yote watakayopewa na viongozi wao kwa kupanda miti mbalimbali iliyokuwa Dodoma.

Aidha, Ametoa Wito kwa Wananchi kupanda miti na kuweza kuitunza ili iweze kupendezesha mandhari ya mji wa Dodoma na kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi. 

"Tunatoa Wito Kwa kila kaya iweze kupanda miti angalau sita (6) pamoja na kuitunza kwa kuimwagilia maji, kuiwekea mbolea na kuzuia mifugo mbalimbali Isiweze kuiondoa",

Mweladzi pia amewasihi wananchi wote wa Dodoma kutokutupa takataka kwenye vyanzo vya mito, makalavati na pia barabarani kwani vitendo hivyo hupelekea uharibufu Wa Mazingira.

No comments:

Post a Comment