NA: WAF, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wazazi na walezi kupeleka Watoto wenye umri kati ya Miezi 9 hadi Miaka 5 katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupata chanjo ya Surua na Rubella katika kampeni maalum itakayoanza Februari 15 hadi 18, 2024
Senyemule ameyasema hayo Leo, katika kikao cha Kamati ya afya Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa mkoa jijini Dodoma, huku akisisitiza kwamba kuzuia magonjwa haya ni jukumu la kila mmoja na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika kampeni za chanjo.
Amesema kuwa chanjo hiyo ambayo inawalenga Watoto wa Miezi 9 mpaka miezi 59 ni hatua muhimu katika kujenga kinga ya mwili dhidi ya magonjwa hatari huku akiwataka wazazi na walezi kuelewa umuhimu wa chanjo hizi na kuacha imani potofu au dhana za kizamani kuhusu chanjo.
Amesisitiza kwamba chanjo ni njia salama na muhimu ya kuzuia magonjwa hatari na kwamba ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote muhimu kulingana na ratiba iliyowekwa na mamlaka husika.
Pia, Mkuu wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano kati ya serikali, watoa huduma za afya, na jamii ili kuhakikisha kuwa chanjo hizi zinawafikia watoto wote kwa ufanisi. Ameelezea kwamba kampeni za chanjo ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na kuhakikisha afya bora kwa watoto.
Mhe. Senyamule, ametoa wito kwa vyombo vya habari na asasi za kiraia kusaidia katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa chanjo na kusambaza habari sahihi kuhusu taratibu za kupata chanjo. Pia, amewaomba viongozi wa dini, wazee wa kimila, na viongozi wa jamii kuchukua jukumu la kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo hizi.
No comments:
Post a Comment