Na. Asila Twaha, Rombo add
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imetoa maelekezo kwa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo waliosimamia mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya na kusema kuwa Kamati haijaridhishwa na usimamizi wa mradi huo na dalili zinaonesha waziwazi kuna ubadhirifu wa fedha.
Kauli hiyo imetolewa mapema Machi 20, 2024 na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC Mhe. Ester Bulaya (Mb) akiwa na wajumbe wa kamati baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa hospitali ya Wilaya ya Rombo na baadae kukagua mradi wa jengo la Halmashauri.
Mhe.Bulaya amesema lengo la kamati ya LAAC ni kuangalia matumizi ya fedha za Umma na ubora wa kazi zilizofanyika katika Halmashauri ambapo ameeleza kusikitishwa kwa miradi ya Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kwa kuchukua muda mrefu, kutokukamilika kwa wakati wakati Serikali ilishawapatia fedha za kutekeleza miradi hiyo.
Akieleza kuonekana kwa dalili za ubadhirifu wa fedha zilizotumika katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya amesema, maelekezo yalitolewa na Serikali na miongozo ya Ofisi ya TAMISEMI ni kuwa shilingi milioni 800 zilitakiwa kujenga majengo manne na badala yake yamejengwa majengo mawili pamoja na Halmashauri kuongeza fedha kutoka mapato ya ndani zaidi ya milioni 170 lakini pia fedha hizo hazionekani matumizi yake.
“mnajiamulia wenyewe kufanya maamuzi yenu hakuna vibali vya kubadilisha matumizi kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuna hospitali zimepewa bilioni 3.1 majengo yote yamekamilika, nyie hamjakamilisha na mmetumia zaidi ya fedha hizo” amesema Mhe. Bulaya
Akisoma mapendekezo ya Kamati Mhe. Abdul (Mb) amesema Kamati imemtaka Mkurugenzi afanye ufuatiliaji wa karibu kwa stoo ya dawa (MSD) ili mashine za kufulia na kupasia ziweze kufungwa kwa ajili ya matumizi ya hospitali kabla ya mwaka wa fedha kwisha, pia Mkurugenzi wa Halmashauri awasilishe taarifa kuhusu mchanganuo wa matumizi ya fedha za hospitali ya Wilaya zilizotoka Serikali kuu na taarifa hiyo iainishe majengo yaliyotakiwa kujengwa kutokana na miongozo ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI
Pia ametaka Mkurugenzi kuainisha sababu za kutokujengwa kwa majengo mawili ya wodi ya upasuaji ya wanaume na wanawake na kufafanua juu ya matumizi ya fedha zilizotakiwa kujenga majengo hayo na kumtaka awasilishe taarifa hiyo kwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kabla ya tarehe 30 April, 2024 .
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Rombo ameishukuru Kamati ya LAAC kwa kufuatilia na kukagua fedha za Umma kwani ni fedha za wananchi huku akieleza wao kama wawakilishi wa wananchi watashirikiana na Halmashauri na kuhakikisha miradi inayoletwa katika maeneo yao fedha zinatu mika kwa usahihi na miradi inakamilika kwa wakati.
No comments:
Post a Comment