Wito umetolewa kwa wakina mama nchini kutumia vipaji vyao walivyobarikiwa na Mwenyezi Mungu ili waweze kujipatia fedha na kujikwamua kiuchumi.
Kamishna Msaidizi Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Bi.Janeth Lewis Hiza ametoa wito huo Machi 10,2024 Jijini Dodoma alipokuwa kwenye hafla ya 'MWANAMKE MWAMBA' msimu wa nne ulio asisiwa na kituo Cha redio Cha C fm 103.3 kilichopo Dodoma, ikiwa ni katika kusherehekea siku ya Wanawake Duniani.
Bi.Janeth amesema wanawake hao hawapaswi kujidharau kwani kuna Hazina kubwa waliyopendelewa na Mungu hivyo wanapaswa kufanya jambo ambalo wameletwa duniani kuja kulifanya kwa juhudi na maarifa.
Kamishna Msaidizi huyo amesema katika nchi yetu ya Tanzania kuna fursa nyingi sana hivyo amewataka wanawake hao kuchangamkia fursa hizo za mikopo kwa kuanzisha vikundi, vikasajiliwa na kusimamiwa na benki kuu ili waweze kufikia malengo yao.
"Hakuna kitu kizuri kama kuwa kwenye Kikundi mpaka ndugu zetu wa PPRA wanatambua vikundi, wakawapa miradi. kwahiyo wakina mama wenzangu tafuteni Marafiki watano waaminifu ili muweze kutumia hizo fursa, Mimi nipo tayari kuwasapoti" alisema Bi.Janeth.
Bi.Janeth amewashawishi wakinamama hao kufungua vituo vya kulelea watoto(Day Care) ili waweze kusaidia kwenye suala la malezi bora kwa watoto.
Aidha,Kamishna Msaidizi huyo
amewataka pia Wanawake hao kuwekeza fedha wanazozipata katika njia mbalimbali za mapato ili waweze kupata mitaji na kufungua Biashara zitakazo wasaidia huko mbeleni.
"Zamani tulikuwa tunategemea kilimo tu ili kuweza kupata fedha, lakini siku hizi tunatafuta pesa kwa njia mbalimbali ikiwemo kilimo, hivyo nikusihi wewe mama, Usile fedha yako yote unayoipata, jitahidi kuwekeza na Baadae hizo fedha uende kuweka Benki ili ziweze kuzaa na wewe kupata mtaji nk." alisema.
Naye Mama mlezi wa kituo hicho cha Redio Mama Tunu Pinda,amewapongeza Wanawake wote walioshinda tuzo ya 'Mwanamke Mwamba' kwa Mwaka huu 2024 na kwa wale ambao hawakushinda,amewataka wasikate tamaa kwani hata mwaka ujao wanaweza kushinda pia.
Kwa upande wake Mkuu wa vipindi C-Fm 103.3 Bw.James Mbonde amesema dhumuni la siku ya 'Mwanamke Mwamba' ni kumpa thamani Mwanamke, kumshika mkono, pamoja na kumtia moyo kwa jitihada mbalimbali ambazo amekuwa akizifanya katika maendeleo ya Jamii na taifa kwa ujumla.
"Sisi Kama kituo Cha Burudani Kanda ya kati na kuelimisha Jamii, tunaamini nguvu ya Mwanamke na mchango wake katika Jamii, na kwa kulithibitisha hilo tumekuwa mstari wa mbele kutumia nguvu na uwezo tulionao kutoa elimu pamoja na kufungua fursa mbalimbali kwa Mwanamke wa Kanda ya kati, pamoja na kuwasaidia baadhi ya Wanawake wenye changamoto mbalimbali na kuwainua kiuchumi" amesema Mbonde.
Naye Mwanamke Mwamba Bi.Anjella Layzer aliyeshinda tuzo ya Mwanamke Mwamba katika kipengele Cha 'Mwamba Katika Chakula' amesema tuzo hiyo aliyoishinda ina maana kubwa sana katika maisha yake na imempa hamasa ya kupambana zaidi katika kitu anachokifanya.
No comments:
Post a Comment