WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amesema bila uhuru, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hawezi kutimiza ipasavyo wajibu wake wa kuhakikisha uwazi na uwajibikaji vinakuwepo katika matumizi ya fedha za Serikali.
Amesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zinapaswa kutambua maeneo yanayostahili kutiliwa mkazo baina ya Serikali, Bunge, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi za Ukaguzi na Mabunge kwenye nchi za SADC (SADCOPAC).
Amesema miongoni mwa maeneo hayo ni kuunga mkono uhuru wa Ofisi ya CAG. “Bila uhuru, CAG hawezi kutimiza wajibu wake ipasavyo katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji wa fedha za Serikali. Kwa hiyo wadau wote wanawajibika kulinda uhuru huu kupitia hatua za kisheria na msaada wa taasisi zenu,” amesema.
Alitoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Aprili 18, 2024) wakati akifunga Mkutano wa Kujenga Uelewa wa Pamoja na Ufanyaji wa Kazi wa Taasisi za Ukaguzi na Mabunge kwenye nchi za SADC (SADCOPAC) uliofanyika kwa siku mbili kwenye hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.
Alisisitiza kuwa suala la kuimarisha uhusiano kati ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (AG) na Bunge ni la muhimu kwani linasaidia kurahisha utendaji kazi baina yao. “Ushirikiano kati ya vyombo hivi unawezesha utendaji na usimamizi rahisi, unaruhusu uchunguzi mzuri zaidi wa matumizi ya fedha za serikali. Ushirikiano huu unaweza pia kuboresha utawala na uwajibikaji ndani ya nchi wanachama,” alisema.
Aliwataka washiriki wa mkutano huo waweke kipaumbele katika kuboresha utawala bora na uwajibikaji kwenye nchi zao. “Kupitia hatua za kisheria na usimamizi, tunapaswa tuhakikishe kuwa mifumo iko sawa na inaweza kuziwajibisha taasisi za Serikali kupitia matumizi yao. Kwa kuzingatia haya, tunaweza kukuza uaminifu kwenye mifumo yetu ya utawala na ustawi wa raia wetu,” alisisitiza.
Katika kusisitiza ushirikiano wa kikanda, Waziri Mkuu aliwaambia washiriki wa mkutano huo kwamba ushirikiano baina ya SADCOPAC na washirika wa kikanda unapaswa kuendelezwa na kuwaahidi kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar imejipanga kikamilifu kufanya kazi bega kwa bega na washirika hao ili kuboresha shughuli za ukaguzi kwenye ukanda huo.
“Serikali imejitolea kusaidia Taasisi Kuu za Ukaguzi (Supreme Audit Institutions), Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PACs) na wadau wengine muhimu ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi bora na ya uwazi ya rasilimali za umma, njia ambayo inakuza utawala bora.”
Mapema, kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Mudrik Ramadhani Soraga alisema Tanzania imefaidika kiuchumi na kimkakati kutokana na mkutano huo kufanyika nchini.
"Wabunge na wawakilishi waliokutana hapa wamejadili mada ambazo zitawawezesha kusaidia Serikali zao katika nchi za SADC kuimarisha uwajibikaji na matumizi mazuri ya rasilimali na mapambano dhidi ya rushwa. Lakini nikiwa Waziri mwenye dhamana ya utalii, mkutano huu umetuongezea mapato,” alisema Soraga.
Naye, Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Dk Othman Abbasi Ali ambaye ofisi yake ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo, alisema mbali na kuimarisha ushirikiano, mkutano wa SADCOPAC umetoa fursa kwa wajumbe wa PAC katika mabunge kubadilishana uzoefu wa njia bora za kufuatilia matumizi bora ya fedha za Serikali kwenye nchi zao.
Naye, Mbunge kutoka Malawi na Mweka Hazina wa SADCOPAC, Mark Botomani, aliwashukuru Marais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka mazingira mazuri yaliyowezesha mkutano huo kufanyika kwa usalama na kwamba Tanzania imekuwa mshirika muhimu wa Jumuiya ya SADC.
Kwa niaba ya wajumbe wenzake wa SADCOPAC, Botomani ameahidi kuwa watafanyia kazi mambo yote waliyojifunza kwenye mkutano huo wa siku mbili ambao awali ulifunguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Mwinyi. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na taasisi za ukaguzi kutoka nchi za SADC.
No comments:
Post a Comment