JAMII YAKUMBUSHWA UMUHIMU WA MALEZI BORA YA FAMILIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 18, 2024

JAMII YAKUMBUSHWA UMUHIMU WA MALEZI BORA YA FAMILIA


Na WMJJWM, Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jonsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameiasa jamii kuona umuhimu wa malezi bora kwa watoto ndani ya familia kama chanzo cha jamii.

Ametoa wosia huo Aprili 18, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa Habari ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia hapo Mei 15, 2024.

Waziri Dkt. Gwajima amesema, Tanzania huungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku hiyo kwa lengo la kutathmini nafasi ya familia katika ustawi na maendeleo yao na mchango wao kwa taifa ambapo mwaka huu 2024 maadhimisho yatafanyika kimikoa kwa kugusa ngazi ya jamii yaani Vijiji, Mitaa na Kata.

Akielezea hali ya sasa kwa mujibu wa utafiti wa hali ya Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria nchini ya mwaka 2022, Dkt. Gwajima amebainisha
mifarakano na migogoro katika familia imesababisha malezi duni na uangalizi hafifu wa watoto hususan watoto wa kike iliyopelekea watoto hao kuanza ngono katika umri mdogo jambo ambalo limesababisha mimba za utotoni kuendelea kuwepo kwa kiwango kikubwa. 

"Asilimia 27 ya wanawake wa umri wa miaka 15 hadi 49 walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili, 12% kati yao walifanyiwa ukatili wa kingono. Vilevile, asilimia 13 ya wanawake waliowahi kuwa na mume katika kipindi cha miezi 12 kabla ya utafiti huo walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili, kingono na kihisia." amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima

Aidha amebainisha kuwa, unyanyasaji wa kimwili, kingono, au kihisia miongoni mwa wanawake walioolewa umepungua kutoka 50% mwaka 2015/16 hadi 39% mwaka 2022/23. 

Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, ukatili wa Watoto Mtandaoni na kwenye familia umechangia kuongezeka kwa migogoro ya kifamilia hususan kati ya wenza au wanandoa jambo lenye athari kubwa katika malezi na ustawi wa watoto wa familia na jamii kwa ujumla. Mfano, watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wengi wamekimbia familia zao kutokana na migogoro ya wenza au wanandoa.

Hata hivyo, Waziri Dkt. Gwajima amefafanua kwamba, Wizara imeendelea kuratibu huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia kupitia Baraza la Usuluhishi wa Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Mabaraza ya Kata na Mabaraza ya Jumuiya ambapo kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 jumla ya mashauri 14,600 yalishughulikiwa yakiwemo migogoro ya ndoa 5,306 (36%), migogoro ya kifamilia na matunzo ya Watoto 5,944 (41%), yaliyohusu matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa yalikuwa 3,350 (23%).

Dkt. Gwajima ametumia nafasi hiyo kuendelea kuwaomba viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kutoa ujumbe mahsusi kuhusu umuhimu wa malezi bora ya watoto katika kujenga familia imara na Taifa imara la Tanzania.

Ametoa wito pia kwa Wakuu wa Mikoa kupitia watendaji ngazi za Halmashauri kuratibu afua za kuelimisha malezi chanya kwa watoto na wazazi au walezi katika ngazi za Jamii ili kukabiliana na changamoto za malezi zitokanazo na matokeo hasi ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano na mwingiliano wa mila na desturi zisizofaa za mataifa mengine. 

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni "Tukubali Tofauti Zetu kwenye Familia; Kuimarisha Malezi ya Watoto." 

No comments:

Post a Comment