Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ameriarifu Bunge wakati akijibu swali la Mbunge wa Hai Mhe. Saashisha Mafuwe bungeni jijini Dodoma leo tarehe 30, 2024.
Katika swali hilo, mbunge huyo alitaka kujua tamko la Serikali kuhusu kuteketeza miti ya mikaratusi nchini baada ya tafiti kuonesha kuwa inaharibu mazingira.
Mhe. Khamis amesema kuwa mara baada ya tafiti kukamilika Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii zitatoa elimu kwa wananchi kuhusu miti hiyo.
Akiendelea kujibu swali hilo naibu waziri amesema kuna zaidi ya spishi 500 za miti ya mikaratusi duniani ambapo Tanzania kupitia TAFORI imeruhusu aina 25 za miti hiyo ili kupata fursa mbalimbali zitokanazo na mikaratusi hasa kwenye viwanda vya mazao yaliyosindikwa.
”Serikali kupitia Wizara ya Maji, Maliasili na Utalii pamoja na sisi Mazingira tumegundua ipo miti inayokunywa maji na inapunguza au kuchangia vyanzo vya maji kupotea, pia tumegundua ziko spishi tofauti kwa mfano ziko zaidi ya 20 na zinatumia maji, hivyo tuko katika mpango wa kuzifanyia tafiti,” amesema Mhe. Khamis.
Hata hivyo, amewahimza wananchi kuendelea kupanda miti kwa wingi wakati Serikali inaendelea kufanya tafiti kuhusu miti ya mikaratusi kubaini athari za kimazingira.
No comments:
Post a Comment