OR-TAMISEMI, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Christopher Ngubiagai amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kuhakikisha wanasimamia kikamilifu matumizi ya mfumo wa Force Account ili kuondoa hoja za ukaguzi katika ngazi ya msingi.
Mhe. Ngubiagai ametoa kauli hiyo tarehe 29 Aprili, 2024 wakati akifunga mafunzo kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata Mkoa wa Mwanza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza jijini Mwanza.
Mhe. Ngubiabai amesema Mfumo wa ‘Force Account’ unahusisha matumizi ya fedha kidogo kwa matokeo makubwa hususani katika kutekeleza miradi ya maendeleo, kutumia mafundi wa kawaida (Local Fundi) pamoja na kuwasimamia kwa kutumia wataalam wa ndani, ni mfumo mzuri ila msipousimamia kikamilifu hautaleta tija na tutaishia kupata hoja.
Mhe. Ngubiabai ameongeza kuwa kiasi kikubwa cha fedha kinapelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za msingi kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya, shule, zahanati na miundombinu mingine lakini ngazi hizo hakuna wataalam wa kufanya manunuzi, Wahasibu na Wahandisi hivyo nyie ndio mnapaswa kuhakikisha kuwa kila kitu kinaenda sawa ili kuondoa hoja za ukaguzi na kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali.
“utaratibu huu wa ‘force account’ umeonyesha manufaa makubwa kwa kutumia fedha kidogo kwa kazi kubwa, yapo maeneo yaliyofanya vizuri sana kupitia utaratibu huo lakini pia yapo maeneo ambayo utekelezaji wake umekuwa ukikabiliwa na changamoto kubwa unaotokana na usimamizi hafifu na kupelekea miradi kukamilika chini ya viwango hivyo thamank ya fedha kukosekana hivyo mfumo wa ‘force account’ ila ongezeni usimamizi’ alisema Mhe. Ngubiabai.
Aidha, ameiomba Ofisi ya Rais TAMISEMI kuangalia uwezekano wa kuwapatia fedha za uendeshaji wa ofisi za Tarafa na Kata ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kwani Ilani ya Chama Tawala ya mwaka 2020 ndio mkataba wao wanaotakiwa kuutekeleza kwa nguvu zote katika kuihudumia jamii inayowazunguka.
Pia amewaasa maafisa hao kutumia nafasi zao kwa kufanyia kazi mafunzo waliyoyapata huku wakizingatia nguzo tano za uadilifu kwa vitendo, uwajibikaji, ubunifu katika kazi, kuwa wasikivu ili kuweza kushauri mambo mbalimbali na kuwa wazalendo kwa kupenda Taifa lao hali wakifanya kazi pasipo mazoea.
Naye Ibrahim Minja Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema mpaka sasa mikoa 18 imepatiwa mafunzo kwa Makatibu Kata 2,574 Maafisa Tarafa 341 na mikoa nane ndiyo iliyobakia ambayo ni Manyara, Arusha, Morogoro, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Tanga, na Ruvuma na matarajio ya Serikali kwa maafisa hao ni kwenda kuboresha utendaji wao wa kazi kwenye maeneo yao kama vile kusimamia miradi ya maendeleo kwa weledi na kutatua kero za wananchi.
No comments:
Post a Comment