WAZIRI BASHUNGWA ATOA MIEZI MIWILI KWA CRB NA NCC KUUNDA MABARAZA YA WAFANYAKAZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, April 22, 2024

WAZIRI BASHUNGWA ATOA MIEZI MIWILI KWA CRB NA NCC KUUNDA MABARAZA YA WAFANYAKAZI


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour anazisimamia Taasisi za Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kuhakikisha zinaunda Mabaraza ya Wafanyakazi ambayo yanaundwa kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004.

Bashungwa ametoa agizo hilo Aprili 22, 2024 jijini Dodoma wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi la Mfuko wa Barabara (RFB) na Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Wizara na Taasisi zake ambapo ameagiza hadi kufikia Juni 30, 2024 Mabaraza ya Taasisi za NCC na CRB ziwe zinafanya kazi kwa mujibu wa Sheria.

“NCC pamoja na CRB kupitia kwa Katibu Mkuu jipangeni nataka hadi kufika Juni 30 nipate taarifa ya Taasisi hizi ziwe na Mabaraza ya Wafanyakazi na yanayofanya kazi”, amesisitiza Bashungwa.



Bashungwa amewataka wajumbe wa Baraza la Bodi ya Mfuko wa Barabara kubuni na kuleta vyanzo vipya vya mapato kwa dhumuni la kusaidia uwepo wa mapato ya kutosha na endelevu kwa ajili ya usimamizi wa matengenezo ya barabara hapa nchini.

Bashungwa amesisitiza kwa wajumbe wa mabaraza kutumia fursa ya uwepo wao katika mabaraza hayo kuhoji na kutoa mapendekezo yatakayokuwa na mchango na kuzaa matunda katika kuiletea nchi yetu maendeleo.


Vilevile, Bashungwa amewakumbusha wajibu wa Baraza la Wafanyakazi ikiwemo Usimamizi wa Rasilimali watu sambamba na kuwajengea weledi, ujuzi na uwezo kwa watumishi pamoja na kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi.

Aidha, Bashungwa ameziagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili wa Makadiriaji Majenzi na Wabunifu Majengo (AQRB) kufuatilia miradi wanayoisimamia kabla ya tatizo kutokea pamoja na kushirikiana na kuchukua hatua kwa watu wanaokiuka maadili ya taaluma zenu.

Kuhusu mfumo wa ufuatiliaji na tathimini, Waziri Bashungwa amewasihi Wakuu wa Taasisi kuboresha majukumu yao ya kiutendaji kupitia mfumo huo ikiwemo kuongeza ufanisi na weledi.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour ameeleeza kuwa Wizara pamoja na Taasisi zake itaanza kutumia rasmi mfumo huu kuanzia tarehe 2 Mei, 2024 ambapo matarijio ya Wizara kupitia mfumo huo utaongeza ufanisi wa Wizara na Taasisi zake na kupunguza matumizi ya fedha za Serikali na kuwezesha kuwa na takwimu sahihi kati ya Wizara na Taasisi zake.

Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Bodi hiyo Mhandisi Rashid Kalimbaga ameeleza kuwa Baraza la wafanyakazi wa Bodi hiyo linajumuisha wajumbe mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Vitengo, Wawakilishi wa Vitengo, Wajumbe wa Halmashauri ya TUGHE tawi la Bodi, Mwenyekiti wa TUGHE kutoka Wizarani, Mjumbe wa TUGHE Taifa na Mjumbe wa TUGHE Mkoa wa Dodoma.

No comments:

Post a Comment