Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Kampuni Tanzu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania T-PESA imetakiwa kuwa kitovu cha ubunifu katika kutoa huduma za kifedha kidigitali nchini.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo Bi. Zuhura Muro wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL PESA LIMITED pamoja na Bodi ya Wadhamini ya TTCL Pesa Trust Entity iliyofanyika Mei 9, 2024 jijini Dar es Salaam.
Bi. Zuhura ameitaka T-PESA kuhakikisha inaongeza ubunifu wa bidhaa na huduma inazozitoa kwa wateja wake ili iweze kutimiza maono ya TTCL ikiwa ni pamoja na kutengeneza faida na kuongeza hisa.
Amesema T-PESA ikiongeza ubunifu zaidi italisaidia Shirika kutimiza maono ya kukamilisha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano ambao unalenga kuchochea mabadiliko katika sekta ya mawasiliano hapa nchini na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uwekezaji kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Bi. Linah Igogo amesema Bodi iliyozinduliwa inapaswa kufanya maamuzi yenye tija ambayo yataiwezesha T-PESA kukua kibiashara na kuwa na mipango madhubuti itakayosaidia kutengeneza faida.
"Ni matumaini yetu kuwa Bodi ya TTCL PESA mmejipanga vizuri ili kuhakikisha Kampuni ya T-PESA inakuza uchumi wa kidigitali na kuongeza mapato ya nchi hivyo ni wajibu wenu kuwa na mikakati ya kuongeza hisa na kupanua wigo wa biashara ili kuongeza faida na kuiwezesha Serikali kupata gawio". Amesema Bi. Linah
Akipokea maelekezo hayo Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya TTCL PESA, Bw. Richard Mayongela amesema Bodi hiyo itatimiza maono ya TTCL ambayo yatasaidia katika utekelezaji wa ujenzi wa uchumi wa kidigitali nchini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Mhandisi Peter Ulanga amesema lengo la TTCL ni kuhakikisha linatoa huduma bora nchini na nje ya mipaka ya Tanzania.
"Malengo yetu ni kuona Tunatoa huduma nzuri za fedha mtandao kwa Watanzania na nje ya nchi yetu". Amesema Mhandisi Ulanga
No comments:
Post a Comment