Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesema Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa kina wa Barabara ya Chanzuru - Melela - Kilosa (km 64.5) imekamilika na sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuijenga Barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya Bungeni jijini Dodoma leo Mei 24, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi aliyeuliza Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Chanzuru hadi Melela - Kilosa itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
"Serikali inapokea ushauri na tuna utaratibu pale tunaposhindwa kupata fedha kwa pamoja kujenga barabara yote huwa tunaanza kuijenga kwa awamu na tukianzia hasa maeneo ya miji na maeneo korofi", amesema Eng. Kasekenya.
Eng. Kasekenya amesema Barabara nyingi zimeharibika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha maeneo mbalimbali nchini ambapo barabara ya Rudewa - Kimamba ni miongoni mwa barabara iliyoharibika na tayari Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro ameshafanya tathmini ya maeneo yote yaliyoharibika ili yafanyiwe marekebisho.
Aidha, Eng. Kasekenya amesema ujenzi wa barabara kwa maeneo mbalimbali nchini ulisimama kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na sio malipo kwa Makandarasi, lakini tayari Makandarasi wameanza kurudi 'site' kukamilisha miradi na wataikamilisha kwa mujibu wa muda uliopo kwenye mkataba.
Eng. Kasekenya amesema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mwita Waitara Mbunge wa Tarime vijijini aliyeuliza nini kauli ya Serikali kufuatia ujenzi wa barabara Tarime Mjini - Nyamongo kusimama?.
"Ni kweli barabara nyingi zilikuwa zimesimama si kwa sababu ya kutokulipwa bali mvua kubwa iliyonyesha na hasa maeneo ya Tarime, nimuhakikishie Mbunge tayari Wakandarasi wote waliokuwa wamesitisha shughuli kwa sababu ya mvua wameanza kurudi na watakamilisha miradi ya ujenzi wa barabara kwa namna tulivyoingia nao makubaliano ya kimkataba", amesema Eng. Kasekenya.
No comments:
Post a Comment