ASILIMIA 89 YA VITONGOJI NKASI VIMEFIKIWA NA UMEME- MHE.SALOME - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 10, 2026

ASILIMIA 89 YA VITONGOJI NKASI VIMEFIKIWA NA UMEME- MHE.SALOME



Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema asilimia 89 ya vitongoji 724 wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa vimesambaziwa umeme, na vitongoji vilivyosalia vitakuwa vimesambaziwa nishati hiyo ifikapo 2030.

Mhe. Salome amesema hayo katika Mji wa Namanyere, Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.

“Sisi Sekta ya Nishati jukumu letu ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata umeme wa uhakika wakati wote. Hapa Nkasi kwa sasa wanatumia umeme kutoka nchini Zambia kupitia makubaliano ya kikanda ya kuuza na kununua umeme ili kuweka mfumo imara wa upatikanaji wa umeme. Hata hivyo, tunatarajia kama kila kitu kitakwenda sawa, Nkasi itapata umeme wa gridi ifikapo mwezi Mei mwaka huu,” amesema Mhe. Salome

Ameongeza kuwa, mradi wa kupeleka umeme wa gridi mkoani Rukwa unaendelea vizuri na mara umeme huo utakapofika mkoani humo, wananchi watanufaika na umeme wa uhakika huku pia wakiwa na nafasi ya kupata umeme wa ziada kutoka nchini Zambia.

 Aidha, kituo cha umeme cha Sumbawanga kinatarajiwa kutumika pia katika biashara ya umeme kwa nchi jirani, ikiwemo Zambia.

Akizungumza na wananchi katika Mji wa Namanyere, Mhe.Salome amewahamasisha kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi kama kuni na mkaa na badala yake watumie nishati safi ya kupikia.

Amesema Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia, ikiwemo kutoa ruzuku ya hadi asilimia 85 kwa majiko banifu na ruzuku ya asilimia 50 kwa mitungi ya gesi ya kilo sita.


No comments:

Post a Comment