NA. MWANDISHI WETU .
Leo Mei 25,2024, ikiwa ni siku ya Afrika,tujadili hili la kilimo na usalama wa udongo Afrika, athari zake bila kusahau utatuzi wake.
Lugha ya sokoni kati ya wauzaji na wanunuzi katika masoko ya kawaida ya watu wa hali ya chini wanaoishi chini ya dola mbili kwa siku barani Afrika sasa hawaongei lugha moja katika maelewano ya mteja na mnunuzi.
Wauzaji wanasikika wakisema siwezi kukupunguzia bei ya kitunguu kwa sababu hata huko ninakovifuata ni adimu,huku wanunuzi wakisema jamani mbona bei ni tofauti na ulivyokuwa unaniuzia zamani? lakini chanzo ni Mafuriko na Ukame,kwani uzalishaji wake umeshuka kutokana na athari hizo.
Ufuatiliaji maalum katika baadhi ya masoko hapa nchini Tanzania ulibaini mabadiliko makubwa ya bei za vitunguu,mfano katika masoko yaliyo mengi Vitunguu Swaumu vimepanda na kufikia shilingi 25,000 kwa kilo moja, ya sokoni imekuwa ya malalamiko zaidi kati ya mteja na muuzaji, mvua kubwa zilizonyesha zikijumuishwa kwenye lawama hizo.
Hali inayopelekea wimbi la hali ngumu ya kiuchumi, matumizi yanazidi kipato na ‘mikopo kausha damu’ inachukua mkondo wake.
Athari zinaelekezwa kwa mtu mmoja mmoja kuanzia kwenye afya ya akili, kwa sababu kwa sasa shilingi 5,000 kwa kilo moja ya vitunguu maji,nyanya ndoo ndogo kabisa shilingi 7,000 ni gharama zinazosababisha msongo wa mawazo kwa watumiaji wa kipato cha chini.
Kupanda huku kwa bei kunakuja huku vipato vya watu vikiwa vimeathirika pia kutokana na majanga hayo ambayo kwa namna moja ama nyingine yameyumbisha hadi uchumi wa nchi za Afrika.
HALI ILIVYO KATIKA NCHI ZA AFRIKA
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa AU, Moussa Faki Mahamat mapema mwezi huu katika Mkutano Mkuu wa azimio la Nairobi kuhusu Mbolea na Afya ya udongo Afrika,alikaririwa akisema kuwa Mafuriko na Ukame unaoushuhudiwa kwa sasa barani Afrika, unatoa angalizo dhidi ya kupungua kwa uzalishaji wa chakula katika sekta ya kilimo jambo linaloweza kuongeza hali mbaya kwa Afrika.
Changamoto za uhaba wa chakula, lishe duni, na mabadiliko ya tabianchi vinaendelea kuwepo na hatua za haraka zikihitajika,aliongeza Mousa Faki Mahamat.
JE WAJUA KUWA UDONGO NAO UNAPASWA KULINDWA?
Kufuatilia athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi zilizotokea katika mataifa ya Afrika Mashariki na kwingineko, Umoja wa Afrika umekuja na kauli mbiu isemayo ‘Kusikiliza Udongo’ katika Mkutano wake mkuu wa wadau wa kilimo na viongozi wa Afrika kuhusu Mbolea na Udongo, uliofanyika Mei 7 hadi 9 jijini Nairobi, Kenya,taifa ambalo lilishuhudia vifo zaidi ya watu 100 kutokana na mafuriko.
Katika taarifa yake mwenyekiti wa Umoja wa Moussa Faki alibainisha kuwa kufuatia athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi ni vyema hatua za haraka zikachukuliwa ili kulinda afya ya udongo.
Uzalishaji wa mazao kupungua katika maeneo mengi duniani ni muhimu sasa kwa bara la Afrika kuwa na mikakati madhubuti ya ulinzi wa ardhi yetu. Na hii ikianzia kwa bara la Afrika lenyewe kuandaa mbolea zetu wenyewe kwa bei nafuu ili wakulima waweze kuzitumia na kurutubisha udongo.
Utumiaji mzuri wa mbolea unaweza kukomboa ardhi ya Afrika na majanga ya asili kama ya mafuriko na mipango endelevu ya kilimo ikaboreshwa zaidi.
UTASHI WA KISIASA UPO VIPI KATIKA KILIMO?
Utashi wa kisiasa ni muhimu katika hatua hii muhimu, ili kudhibiti mianya inayoathiri afya ya udongo,alisisitiza Faki.
Hata hivyo hivi karibuni kumekuwa na Sakata la mbolea bandia ama feki nchini Kenya, huu ukiwa ni mfano hai kuwa mbolea asilia na zenye bei nafuu ni muhimu katika sekta ya kilimo na utekelezaji wa maazimio lazima ufikiwe kwa wakati.
Naye rais wa mkutano huo na mwenyeji wa mkutano huo rais wa Kenya William Ruto alisisitiza umuhimu wa utatuzi wa tatizo hilo la udongo kwa haraka.
Rais Ruto alisema barani Afrika watu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, katika kuwekeza kwenye kilimo, hii ikijumuisha matumizi ya mbolea, mabadiliko ya hali ya hewa na udongo kukosa afya.
AFRIKA INA MPANGO GANI KATIKA KILIMO?
Mpango wa Agenda ya mwaka 2063, kuwa Afrika inapaswa kutatua matizo yake , ni rahisi na muhimu kwa kuwa Waafrika wanajua matatizo yao wenyewe zaidi ya mtu mwingine yeyote nje ya Afrika.
Ni vyema kuwa na malengo na mipango mikakati ya utekelezaji wa pamoja ili kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo na kuwapa unafuu wa maisha wananchi wa bara la Afrika.
‘Listen to the soil’ unaweza kuwa mwanzo mzuri katika kulibadilisha bara la Afrika kuwa mzalishaji mkubwa katika sekta ya kilimo, kutoa ajira, kutengeneza utajiri na kuwa msambazaji mkubwa wa chakula dunian,ni jambo linalowezekana iwapo tu kutakuwa na mipango madhubuti na utashi chanya wa kisiasa.
MAAZIMIO MENGINE YA KILIMO AFRIKA
Azimio la Nairobi, limekuja wakati ambapo bara hili likiwa limepita katika maazimio kadhaa wa kadhaa, Azimio la Abuja la 2006 kuhusu Mbolea kwa ajili ya Mapinduzi ya Kijani, likibainisha umuhimu wa kuongeza matumizi ya mbolea ili kuchochea ukuaji wa tija ya kilimo kwa lengo la kutokomeza njaa na umaskini barani Afrika.
Azimio la Malabo la Programu ya Maendeleo ya Kilimo Afrika lililopitishwa wakati wa Mkutano wa Kawaida wa 33 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika mjini Malabo, Equatorial Guinea mwezi Juni 2014. Katika Azimio hilo, Nchi Wanachama waliahidi kuwa na mabadiliko jumuishi ya kilimo.
Azimio la Maputo la mwaka 2003 ambalo liliangazia changamoto za kutekeleza Maendeleo Jumuishi na Endelevu katika Kilimo na Maji barani Afrika, changamoto za kudumu na za muda mrefu katika kutekeleza ahadi katika maazimio mbalimbali na kuthamini maendeleo yaliyofikiwa tangu Azimio la Abuja.
Viongozi na wadau wa kilimo Afrika, wameangazia Azimio la Nairobi katika utegemezi unaoendelea kwenye kuboresha ardhi ya kilimo ili kuongeza uzaishaji wa kilimo, kasi ndogo inayoendelea ya ongezeko la tija ya kilimo, eneo dogo lililo chini ya usimamizi endelevu wa udongo na matokeo ya kupungua kwa virutubishi vya udongo, mapato madogo ya mkulima, uharibifu mkubwa wa ardhi, uzalishaji wa hewa ya Kaboni, upoteaji mkubwa wa bayoanuwai, na gharama kubwa ya kimazingira vinachangia katika matatizo ya sekta ya kilimo.
Haja ya ushirikiano wa kikanda kuhusu suala la mbolea na afya ya udongo ni kubwa kuliko ilivyokuwa hapo awali kwa vile fursa za uwekezaji na biashara ni muhimu miongoni mwa nchi za Afrika.
Ikumbukwe pia mfumo wa uwasilishaji bidhaa kwenda kwa mtumiaji wa mwisho barani Afrika ni dhaifu, huku kukiwa na umbali mrefu kwa wakulima kupata mbolea na pembejeo zingine muhimu za kilimo pamoja na huduma za ushauri,jambo ambalo kama halitatatuliwa bado ni ndogo kwa Afrika kujikwamua katika sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment