Baada ya miezi kadhaa ya mabishano na changamoto za kisheria bado zinaendelea, Kenya imetuma kikosi chake cha kwanza cha maafisa 400 wa polisi kukabiliana na ghasia za magenge nchini Haiti.
Kutokana na kutikiswa na miongo kadhaa ya ukosefu wa utulivu, taifa hilo la Karibean limeshuhudia kuongezeka kwa ghasia kufuatia mauaji ya Rais Jovenel Moïse miaka mitatu iliyopita.
Makundi hasimu yenye silaha yalichukua udhibiti wa mji mkuu, Port-au-Prince, mapema mwaka huu, na kumlazimisha Waziri Mkuu Ariel Henry kujiuzulu wiki kadhaa baadaye.
Magenge yenye silaha sasa yanadhibiti takriban 80% ya jiji.
"Matumizi madhubuti ya nguvu" yanahitajika kukabiliana nao, unasema Umoja wa Mataifa, ambao umeidhinisha ujumbe wa polisi unaojumuisha maafisa 2,500 kutoka mataifa mbalimbali - ikiwa ni pamoja na 1,000 walioahidiwa na Rais wa Kenya William Ruto.
Lakini kuna upinzani mkali nyumbani kwa uamuzi wa Bw Ruto - kwa sababu polisi wa Kenya wanalaumiwa kwa kufanya dhuluma katika nchi yao.
Wakifanya kazi na polisi wa Haiti, na wenye makao yake makuu katika kambi iliyojengwa na Marekani, maafisa wa Kenya watalenga kurudisha maeneo muhimu ambayo yamekuwa chini ya udhibiti wa magenge, ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa karibu na bandari za baharini.
Haiti haijafanya uchaguzi tangu 2016.
Kwa hivyo uchaguzi unapaswa kupangwa ndani ya mwaka mmoja, na kuruhusu hilo kutokea, ujumbe unaoongozwa na Kenya unapewa jukumu la kurejesha usalama.
Kutumwa kwao kumeidhinishwa kwa mwaka mmoja, na uhakiki utafanywa baada ya miezi tisa.
No comments:
Post a Comment