Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI haitasita kuchukua hatua kwa kiongozi yeyote anayewanyanyasa wananchi kupitia ukusanyaji wa ushuru wa mazao kwani Serikali imeshakwisha kutoa Miongozo kuhusu ukusanyaji wa ushuru wa mazao.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo wakati akichangia hoja yake bungeni jijini Dodoma katika Bunge la Bajeti ya mwaka 2024/2025 linaloendelea.
“yapo maeneo ambapo tunaona kuna hitulafu katika ukusanyaji wa ushuru wa mazao, tutafika huko katika Halmashauri zenye changamoto hizo, maelekezo yangu watanzania wasiyanyasike kwenye maeneo yao na TAMISEMI hatutasita kuchukua hatua kwa kiongozi yeyote anawanyanyasa Watanzania katika maeneo yetu kwani serikali ilikwisha kutoa muongozo”
Aidha Mhe. Mchengerwa amesema ifikapo tarehe 30 mwezi juni maandalizi juu ya utolewaji wa Mikopo ya asilimia 10 yatokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri yatakuwa yamekamilika na wataalamu kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI watafika katika Halmashauri zote nchini ili kutoa elimu ya utaratibu ulioboreshwa katika utolewaji wa Mikopo hiyo ili wanufaika wa mikopo hiyo wawezekunufaika.
Amesema Serikali imetenga zaidi ya Bil. 400 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya katika kila jimbo la uchaguzi kote nchini na kwaajili ya kujenga na kukarabati Hospitali za Halmashauri.
Pia Mhe. Mchengerwa ameunga mkono hoja ya Bajeti iliyotolewa na Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo aliyoitoa leo Bungeni Jijini Dodoma katika Bunge la Bajeti linaloendelea.
No comments:
Post a Comment