KUOGA BARAFU NA KUFANYA MAZOEZI: MAISHA YA MRENO CRISTIANO RONALDO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 2, 2024

KUOGA BARAFU NA KUFANYA MAZOEZI: MAISHA YA MRENO CRISTIANO RONALDO

 

Fonte akiwa juu ya Ronaldo wakati wakishangilia ushindi wa Ureno kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Poland katika robo fainali ya Euro 2016

Huwa nacheka ninaposikia hadithi na uvumi kuwa uwepo wa Cristiano Ronaldo katika kambi ya timu ya Ureno, huleta usumbufu - kwa sababu sio kweli - ni hadithi tu.


Nilikaa naye kwa miaka mingi kwenye timu ya taifa na sikuwahi kuona matatizo yoyote. Ninachojua, sio tu ni mchezaji mkubwa, pia hujaribu kumsaidia kila mtu katika kikosi.


Hata kumfuatilia tu kunaweza kukupa mawazo ya nini unapaswa kufanya ili ufanikiwe, na unapokuwa na Cristiano unapata mengi zaidi ya kujifunza.


Yeye ndiye nahodha wa kikosi na amekuwa akipaza sauti yake, huzungumza sana, iwe ndani au nje ya uwanja na huzungumza kwa mifano pia.


Huenda mapema kuliko kila mtu kwenye mazoezi, na hufanya mazoezi yake ya mwili na kuutayarisha mwili na akili yake.


Huongoza, nasi tunafuata. Nakumbuka sote tulijiroweka kwenye barafu na kwenda kwenye sauna saa 2 asubuhi kwa sababu yake, na ilisaidia mwili kupona. Jambo muhimu ni kwamba tulikuwa tukifanya pamoja, kikosi kizima.


Pamoja na kuipa timu ari, pia ni fursa ya kujifunza kutoka kwa walio bora zaidi. Cristiano ana uwezo wa kuzungumza kwa ujuzi mkubwa sana - na jambo zuri ni kwamba anafurahi kushirikiana na kila mtu.





Nimemjua Cristiano kwa muda mrefu, tangu tulipokuwa pamoja tukiwa vijana katika timu ya Sporting, na sikuzote alionyesha hamu ya kutaka kuwa bora zaidi.


Alikuwa akicheza nami katika timu ya vijana wasiozidi umri wa miaka 17 alipokuwa na umri wa miaka 16. Alikuwa tayari ana kipaji kikubwa, na kila mtu pale Sporting alitambua kuwa ana kitu cha kipekee.


Pamoja na uwezo wake, daima ungemuona akiinua vyuma baada ya mazoezi, akijaribu kuupa mwili nguvu na kuwa mwepesi wakati kila mtu alikuwa tayari ameshakwenda nyumbani.


Daima alikuwa akitaka kushinda. Alikuwa mshindani sana. Akitwambia nataka kufanya pushapu nyingi kuliko mtu yeyote baada ya mafunzo, na bila shaka alifanya hivyo.


Shauku yake ndio imemfanya hadi sasa yupo kwenye Euro 2024 akiwa na Ureno, akiwa na umri wa miaka 39. Ni mnyama anaetaka kuendelea kushinda na kushinda. Sio tu ni bora, hutaka kuthibitisha ubora wake.


Kuwa na mawazo ya kutaka kubaki katika kiwango chako kwa miaka mingi, ni jambo gumu sana, kwa sababu inahitaji kazi kubwa sana.


Huyo ndiye Cristiano. Ndio maana ameshinda sana na kufanya mengi. Na kati ya mambo mengi yanayomfanya kuwa mchezaji na mtu bora, naweza kusema ni nguvu zake.


Nilikuja kwenye kikosi cha Ureno nikiwa na karibu miaka 31 - nilipoitwa mwaka 2014 - lakini kwa miaka minane iliyofuata nilikuwa na wakati mzuri na Cristiano.


Nina kumbukumbu nzuri, kubwa zaidi ni Ureno iliposhinda Euro 2016.


Unapaswa kukumbuka jinsi tulivyoanza mashindano hayo, tukiwa na sare tatu dhidi ya Iceland, Austria na Hungary kwenye kundi letu.


Baada ya sare na Hungary tulijua tumefuzu, lakini kila mtu hakuwa na furaha na kila mtu akasema kile alichofikiri kinahitajika kufanywa.


Kwa sababu ya umoja wetu, tukawa na kiwango kikubwa sana cha ushindani. Katika mazoezi, ilikuwa kama tunacheza michezo.


Wachezaji ambao walikuwa hawatumiwi sana walikuwa wakifanya mazoezi kwa shauku kubwa na walihakikisha wako tayari ikiwa wataitwa.


Tulipopita hatua ya mtoano, imani yetu na kujiamini viliongezeka na kisha safari ikakamilika tulipoifunga Ufaransa katika fainali.


Nikiwa na Cristiano kwenye timu, nilihisi tunaweza kuishinda timu yeyote, lakini alijeruhiwa mapema. Kila mtu katika timu alisema, "sikiliza, itabidi tupambane sana." Ilikuwa kazi ngumu sana, lakini tuliifanya.





Huu ni wakati wa furaha sana na natumai Ureno wanaweza kubeba ubingwa katika michuano hii pia, kwa sababu wana kikosi kizuri sana.


Kwa kile nilichoona kwa Cristiano huko Ujerumani, atasaidia pa kubwa kufanikisha hilo. Katika michezo ya makundi uchezaji wake ni mzuri, amekuwa kwenye nafasi nzuri na amepata nafasi.


Ninajua kwake kusaidia kufunga bao wakati mwingine hujihisi bora kuliko kufunga mwenyewe. 


Kwa hivyo sikushangaa alipochagua kumpasia Bruno Fernandes kwa bao letu la tatu dhidi ya Uturuki badala ya kupiga shuti mwenyewe.


Amehusika kila mahali, akisaidia kulinda na kucheza katikati. Bila shaka anataka bao lake pia kwa sababu ya njaa yake, lakini litakuja - ni suala la muda tu.


Mara nyingi huulizwa; Cristiano ana maana gani kwa Ureno? Nasema, sio tu ni mchezaji wetu bora, ni mchezaji bora zaidi.


Ndiye bendera ya Ureno, mtu anayefuatiliwa zaidi ulimwenguni na hawezi kwenda popote bila kujuulikana.


Lilikuwa jambo jema kuwa naye kwenye kikosi cha taifa kwa sababu kila tulipokwenda, kila mtu alikwenda kwake. Kila mtu hupiga yowe 'Ronaldo.’


Tuna bahati kuwa naye na wachezaji wengine wakubwa kama Pepe ambao wamekuwepo na kushinda – na kutoa ujuzi wao kwa vijana wadogo kwa sababu hilo ni muhimu.


Tuna kikosi bora lakini tunachohitaji ni watu kuendelea na maadili yale yale waliyonayo wachezaji wakubwa, ili kuweka mazingira mazuri kwenye michuano hii na ijayo.


Jambo la muhimu katika soka ni kuwa na timu inayocheza pamoja katika ulinzi au ushambuliaji. Ikiwa utafanya hivyo, una nafasi ya kushinda.

No comments:

Post a Comment