RAIS SAMIA AIELEKEZA TANROADS KUTOA KIPAUMBELE KWA WAKANDARASI WAZAWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, August 4, 2024

RAIS SAMIA AIELEKEZA TANROADS KUTOA KIPAUMBELE KWA WAKANDARASI WAZAWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na viongozi wengine wa Serikali akishangilia mara badaa ya kuvuta kitambaa kuashiria ufunguzi wa barabara ya Rudewa - Kilosa (km 24) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, tarehe 03 Agosti, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa pamoja na viongozi wengine wa Serikali akikata utepe kuashiria ufunguzi wa barabara ya Rudewa - Kilosa (km 24) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, tarehe 03 Agosti, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa katika hafla ya ufunguzi wa barabara ya Rudewa - Kilosa (km 24) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, tarehe 03 Agosti, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima katika hafla ya ufunguzi wa barabara ya Rudewa - Kilosa (km 24) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, tarehe 03 Agosti, 2024. Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Rudewa - Kilosa (km 24), iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, tarehe 03 Agosti, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuendelea kutoa kipaumbele kwa Wakandarasi Wazawa katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara na madaraja ili kuwajengea uwezo na kufanya uchumi kuwa na mzunguko mzuri ndani ya nchi.

Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo Kilosa Mjini  Agosti 03, 2024 katika hafla ya ufunguzi wa wa barabara Rudewa - Kilosa (km 24) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami Mkoani Morogoro. 

"Niwaagize TANROADS kwa yale ambayo Wakandarasi Wazawa wanayaweza wapeni kazi hizo, kwa kuwa ukimpa kazi Mkandarasi mzawa na ukimlipa atakwenda kununua bidhaa kwenye maduka na pesa itazunguka humo humo lakini na yeye atalipa kibarua na fedha itazunguka humo humo”, amesema Dkt. Samia.

Aidha, Dkt. Samia ameeleza kuwa Morogoro ni mkoa wa kimkakati kwa maendeleo ya miundombinu ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu Serikali kupitia TANROADS imeupatia Mkoa huo kiasi cha Shilingi Bilioni 78.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara na madaraja.

Dkt. Samia ameeleza kuwa umuhimu wa mradi wa barabara ya Rudewa - Kilosa kwa wananchi ikiwemo kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na bidhaa na hivyo kuchochea uchumi wa Wananchi wa Kilosa Mjini na kukuza biashara.

Dkt. Samia ameeleza kuwa Serikali inakwenda kukamilisha ujenzi wa barabara katika kipande kilichobakia cha kuunganisha Wilaya ya Kilosa na Mikumi katika barabara ya Dumila – Kilosa – Ulaya – Mikumi (km 142) kwa kiwango cha lami katika mradi huo.

Vilevile, Dkt. Samia ameipongeza Wizara ya Ujenzi, TANROADS na Wakandarasi Wazawa waliotekeleza na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Rudewa - Kilosa (km 24) kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Shilingi Bilioni 45.6.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameeleza kuwa barabara ya Rudewa - Kilosa (km 24) ni sehemu ya barabara muhimu kwa kuwa inaunganisha Mkoa wa Tanga, Morogoro na Nyanda za Juu Kusini ambapo inaanzia Bandari ya Tanga - Handeni - Mziha - Turiani - Dumila - Kilosa - Mikumi - Ifakara - Mlimba - Lupembe hadi Mkoani Njombe.

Bashungwa ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi imetengewa zaidi ya Bilioni 800 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya barabara iliyoathirika kutokana na mvua za El-Nino katika mikoa yote nchini kipindi hiki cha kiangazi ambapo hivi sasa kazi za manunuzi zimeanza kwa ajili ya utekelezaji na Mkoa wa Morogoro ukiwemo.

Awali akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta ameeleza barabara ya Dumila – Kilosa – Ulaya - Mikumi (km 142) ni barabara ya Mkoa inayounganisha barabara kuu ya Morogoro – Dodoma katika eneo la Dumila na barabara kuu ya TANZAM katika eneo la Mikumi.

Besta ameeleza ujenzi wa barabara ya Rudewa - Kilosa umetekelezwa na kampuni ya wazawa ya M/s Umoja Kilosa JV yenye muunganiko wa Makandarasi saba (7) Wazawa na Mhandisi Mshauri kampuni ya PIDAEL JV Consulting Engineers ya Tanzania kwa gharama ya Shilingi Bilioni 45.6 zikihusisha gharama za fidia, ujenzi na usimamizi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi

No comments:

Post a Comment