Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa waratibu na wasimamizi wa miradi inayosimamiwa na kutekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kumalizika kwa wakati ili iweze kusaidia wananchi kama Serikali ilivyokusudia.
Dkt. Kijaji ameongea hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi inayosimamiwa na kutekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Pemba, Septemba 24,2024 ambapo alikagua Mradi wa kuimarisha Miundombinu ya Fukwe, Sipwese, Mkoa wa Kusini Pemba pamoja na Kutembelea Mradi wa jamii wa ujenzi wa ngazi Shehia ya Kizimbani, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema kila mmoja anapaswa kusimamia vyema eneo alilopewa ili kukamilisha kwa wakati miradi hiyo na wananichi waweze kunufaika nayo kwa kufanya shughuli zao za kawaida.
“Viongozi wetu wanatupenda ndio maana leo nimetumwa hapa ili kuangalia kinachoendelea, hivyo nitoe wito kwa wasimamizi wa miradi kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi hii na itakapokamilika kila mmoja anaowajibu wa kuilinda,” amesema Dkt. Kijaji.
Ameongeza eneo la Sipwese ambapo linajengwa tuta la kuzuia maji ya bahari kumekuwa na mmomonyoko ambao umeanza kuleta athari katika baadhi ya maeneo kwa kusababisha uharibifu wa miundombinu iliyopo kama vile barabara, majengo, makazi ya watu na madaraja hali iliyosababisha Serikali kutumia fedha katika kukarabati miundombinu iliyoharibiwa.
Katika Mradi wa Utekelezaji wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini Shehia ya Kizimbani Mhe. Dkt. Ashatu amesema madhumuni ni kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu, pamoja na kusaidia kujenga rasilimali watu hasa watoto kwa kuwapa elimu, huduma za afya na lishe bora.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Wete Mkoa Kaskazini Pemba, Dkt. Hamad Omar Bakari amesema walengwa wa Shehia ya Kizimbani pia wamebahatika kupata mafunzo maalumu ya siku saba ya ruzuku ya uzalishaji, kuandaa mipango ya rahisi ya biashara. Vile vile kaya zilishiriki zoezi la uhakiki wa kaya zilizoboreka kiuchumi.
Kwa mwaka wa Fedha wa 2023/2024 mradi uliyotekelezwa Ujenzi wa vidaraja vya kushukia/kupandia kwa waenda kwa miguu, mradi ambao una urefu wa mita 82, aidha kukamilika kwa mradi huu kumewezesha wananchi ambao wanafanya shughuli zao za kilimo kufika kwa urahisi katika mashamba yao.
No comments:
Post a Comment