Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini (Mb ) amesema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakuna mtu yeyote yule anapaswa kupoteza Haki za Binadamu mwingine ikiwa ni pamoja na kupoteza uhai.
Mhe. Sagini amesema hayo Septemba 19, 2024 wakati aliposhiriki katika Mahafali ya 15 ya shule ya awali na msingi ya Blessed Edmund yaliyofanyika katika ukumbi wa shule hiyo wilaya ya Butiama, Mkoani Mara.
Sagini amesema pamoja na mambo mengine dhana ya utu na haki za kila Mwananchi lazima iheshimiwe na hivyo kila Mwananchi ambaye anataarifa za wahalifu aripoti katika mamlaka husika
"Nataka niwashauri Wananchi Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni alizungumza kwa hisia mambo ya mauji ya raia wasio na hatia na kinyume cha Sheria watu kujichukulia Sheria mkononi lakini matukio yanayokiuka maadili ya Taifa letu, matukio yanayohusishwa na imani za kishirikina amekemea vikali kwa kutumia Maneno Mazito."
Aliendelea kusema "Kama wafanya uhalifu wapo miongoni mwetu kama wanajamii tunawajibu wa kuwafichua ili vyombo vya dola viwachukulie hatua.
Wakamatwe,wachunguzwe na hatimaye wakidhibitika ushahidi ukawatia hatiani wawajibishwe kwa mujibu wa Sheria."Alisema Naibu Waziri Sagini
Aidha, Sagini amewataka Wanafunzi waliohitimu kuhakikisha wanasimamia maadili waliyoyapata walipokuwa shuleni kwa kuwa na mwenendo mwema.
Awali, Mkurugenzi wa Shule hiyo ambaye ni Paroko wa Parokia ya Kiabakari Fr.Wojciech Adam amesema kuwa kanisa kushirikiana na Serikali ya Poland wakiwa wadau wa maendeleo imeendelea kutafuta wafadhili mbalimbali ili kuwekeza miundombinu ikiwemo katika sekta ya Afya na Elimu hivyo amewataka Wazazi kushiriki katika kuchangia matumizi ya kila siku ya shule ili kufanya huduma hiyo kuwa endelevu na kuondoa falsafa ya kutegemea Serikali au Wafadhili pekee.
No comments:
Post a Comment