Na Benny Mwaipaja, Baku, Azerbaijan
Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, ameihamasisha sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo wa kimataifa kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania katika sekta ya uchumi wa buluu kwa faida za kiuchumi na hifadhi ya mazingira ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Mpango ametoa wito huo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akifungua mkutano wa kunadi fursa za uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu zilizopo Tanzania, ulioandaliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tanzania na Wizara ya Uchumi wa Buluu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku, nchini Azerbaijan.
Mkutano huo wa kunadi fursa za uwekezaji katika Sekta ya Uchumi wa Buluu uliandaliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tanzania na Wizara ya Uchumi wa Buluu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya, Shirika la Chakula Duniani (FAO), Shirika la Hifadhi ya Maliasili (IUCN) na mashirika mengineyo.
Dkt. Kijaji alisema kuwa kuwekeza katika shughuli endelevu za uchumi wa bluu na miradi ya kurejesha, kama vile marejesho ya mikoko, miamba ya matumbawe na Bahari, uhifadhi wa maeneo ya mvua na kilimo cha mwani kinaweza kuongeza utenganishaji wa kaboni na kusaidia malengo ya kukabiliana na athari hasi za mabadiliko ya tabianchi kama ilivyoainishwa katika Itifaki ya Kyoto na Mkataba wa Paris.
Aliyataja maeneo ya uwekezaji kuwa ni pamoja na uchimbaji wa madini, uvunaji wa mafuta na gesi, ujenzi wa bandari kavu, uvuvi mkubwa katika kina cha Bahari katika eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 223,000.
Alisema kwamba uwekezaji huo utachangia kukuza uchumi wa nchi na wawekezaji, lakini pia utakuza ajira kwa makundi ya watu wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini na vyanzo vingine vya maji.
Dkt. Kijaji alibainisha kuwa Tanzania imeendelea kujenga miundombinu wezeshi ya kurahisisha ufanyajikazi katika sekta ya uchumi wa buluu ikiwemo kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya Bahari ili kuyaongezea thamani ikiwemo zao la mwani na kujenga viwanja vya ndege na bandari Visiwani Zanzibar na mikoa ya Kusini.
Wakizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi-Zanzibar, Bw. Zahor Kassim El Kharousy, walieleza umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu ikiwemo upatikanaji wa kodi pamoja na maendeleo ya watu.
Zaidi ya watu 200 toka mataifa mbalimbali wakiwemo viongozi waandamizi kutoka Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya, Shirika la Chakula Duniani (FAO), Shirika la Hifadhi ya Maliasili (IUCN) na mashirika mengineyo ambapo waliahidi kuendelea kusaidiana na Tanzania kwenye upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya masuala ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya Tabia nchi kwenye sekta ya Uvuvi nchiniTanzania.
Zaidi wa watu elfu 50, wakiwemo wanadiplomasia kutoka zaidi ya nchi 200 wanachama wa Umoja wa Mataifa, wanakutana katika Jiji la Baku, nchini Azerbaijan wakijadili namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutafuta vyanzo vya fedha za uhakika za kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya kukabiliana na changamoto hizo.
No comments:
Post a Comment