Na Dotto Kwilasa, DODOMA
MTANDAO wa Jinsia Tanzania(TGNP) umefanya kikao kazi cha kuwezesha Menejimenti ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (NAOT) kuzingatia masuala ya kijinsia wakati wa kufanya ukaguzi ili kuimarisha uelewa wa masuala ya Jinsia.
Akizungumza November 28,2024 Jijini Dodoma kwenye kikao hicho Mwezeshaji kutoka TGNP Mary Nsemwa amesema mbali na kuimarisha uelewa wa usawa wa kijinsia mafunzo hayo pia yataimarisha uelewa wa namna ya kuweka vipaumbele vya kijinsia katika mipango na bajeti kwa kuzingatia malengo, Sera, miongozo na kuweka kwenye nyenzo za ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
Ametaja malengo mengine kuwa ni pamoja na kujadili umuhimu wa kuzingatia usawa na kuwa na mtazamo wa kijinsia katika uandaaji wa mipango, miongozo na shughuli za NAOT kama inavyoelekezwa kwenye mwongozo wa bajeti ya mwaka 2024/25.
"Mafunzo haya ni muhimu kwa kuwa yatashirikisha uzoefu wa kitaasisi kuhusu masuala ya kijinsia yatakavyokelezwa kupitia miongozo ya NAOT na changamoto zake ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya utekelezwaji na kuboresha maeneo muhimu ya kijinsia katika mipango, bajeti na uandaaji wa Sera, "amefafanua
Amesema ikiwa Ofisi hiyo itafanya ukaguzi unaozingatia jicho la jinsia itasaidia fedha na rasilimali za umma kutumiwa kwa usawa na haki kwa makundi yote, ikiwa ni pamoja na wanawake, wanaume, na makundi mengine yenye mahitaji maalum.
"Ukaguzi wa aina hii unahakikisha kwamba sera, miradi, na huduma za serikali zinachangia kupunguza au kuondoa tofauti za kijinsia, na kuwa na athari chanya kwa wanawake na wanaume kwa njia sawa.
Mbali na hayo Nsemwa ametaja maeneo ambayo yanapaswa kutazamwa wakati wa kuchunguza kuwa ni pamoja na Ulinganifu wa Bajeti kwa kuchunguza kama bajeti za serikali zinatengwa kwa usawa kwa miradi inayolenga kufadhili masuala ya jinsia, kama vile elimu kwa wasichana, huduma za afya za uzazi, na miradi ya kiuchumi kwa wanawake.
Eneo lingine ni Usawa katika Ajira na Utumishi wa Umma ambapo NAOT inapaswa kuchunguza kama kuna usawa katika ajira, na ikiwa wanawake na wanaume wanapata fursa sawa katika serikali na sekta za umma ikiwa ni pamoja na kuangalia kama miradi na programu za serikali zinachukua hatua madhubuti za kuondoa ukosefu wa usawa wa kijinsia na kuzingatia mahitaji ya kila jinsia.
"Ufanisi wa Sera za Jinsia unatathmini kama sera za serikali zinazohusiana na jinsia zinatekelezwa kwa ufanisi, na ikiwa zinaathiri jamii kwa usawa, bila kupendelea kundi moja kwa lingine na ukaguzi huu unasaidia kuondoa vikwazo vya kijinsia na kuboresha ufanisi wa matumizi ya rasilimali za umma kwa wote, "amesisitiza.
Kwa upande wake Mwezeshaji kitoka TGNP Deugratius Temba amesema ameeleza kuwa mbali na kuwa mlengo wa usawa wa kijinsia ni muhimu kwenye,Jamii inapaswa kujua kuwa mlengo huo haupo kwa ajili ya kumpindua mwanaume bali ni kuweka usawa katika jamii kwenye nyanja za elimu,afya, maji na masuala mengine muhimu.
Amesema Tanzania inaongozwa na miongozo ya usawa wa kijinsia japo utekelezaji wake bado unasuasua na hivyo kusisitiza kuwa bajeti yenye mtazamo wa kijinsia ni muhimu kwani italeta tija na kuibua vipaumbele muhimu kwenye jamii.
Amesisitiza kuwa kwa suala la mgawanyo wa kazi kijinsia linahusu jinsi majukumu na shughuli katika jamii yanavyogawanywa kulingana na jinsia na kwamba hali hiyo inaweza kuonekana katika maeneo mbalimbali kama vile familia, sekta ya kazi, na jamii kwa ujumla. Kwa mfano, wanawake mara nyingi wamepewa jukumu la shughuli za nyumbani kama vile utunzaji wa familia na kazi za nyumba, wakati wanaume wanahusishwa zaidi na kazi za kulipa, kama vile kazi za ofisini, ujenzi, na biashara.
"Mgawanyo huu wa kazi kijinsia ni matokeo ya mifumo ya kijamii, tamaduni, na mila ambazo zinadumisha nafasi maalum kwa kila jinsia. Hata hivyo, mabadiliko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi yanaendelea kuwepo, na kumekuwa na juhudi nyingi za kupunguza au kubadilisha mgawanyo huu ili kutoa usawa na fursa sawa kwa kila jinsia, "amesisitiza
Amesema,kutotekelezwa kwa miongozo ya usawa wa kijinsia ni changamoto kubwa katika jamii inayitokana na ushikiliaji wa Mila na Tamaduni katika maeneo mengi na kufafanua kuwa tamaduni na mila za kijamii zinadumisha mgawanyo wa kazi kulingana na jinsia, ambapo wanaume na wanawake wanatakiwa kutekeleza majukumu maalum.
"Jambo hilii linakuwa gumu kubadili kwani jamii inaweza kuwa na imani za kijinsia ambazo zinaona kuwa baadhi ya kazi au nafasi ni za wanawake au wanaume pekee,ukosefu wa Elimu na Ufahamu katika baadhi ya maeneo ni kichocheo kikubwa cha ukosefu wa usawa hii inaweza kusababisha kupuuza au kutotekeleza ipasavyo miongozo ya usawa wa kijinsia kwa sababu ya ukosefu wa uwelewa wa haki za wanawake na wanaume, "amesema na kuongeza;
Baadhi ya miongozo na sheria zinazohusiana na usawa wa kijinsia zinahitaji rasilimali za kifedha na kibinadamu kwa ajili ya utekelezaji,hata hivyo, katika baadhi ya jamii, kuna ukosefu wa rasilimali za kutosha kuleta mabadiliko haya na kuhakikisha utekelezaji wa miongozo ya usawa wa kijinsia, "amesema.
Mbali na changamoto hizo ametaja vikwazo vya Kisheria kuwa vinakwamisha juhudi za wadau na kueleza kuwa ingawa miongozo ya usawa wa kijinsia ipo, kuna mifumo ya kisheria na taratibu ambazo haziungi mkono au hazifuatilii utekelezaji wa sheria za usawa wa kijinsia, jambo ambalo linaweza kusababisha kushindwa kwa hatua za utekelezaji.
"Hivyo, ingawa kuna juhudi za kisera na kisheria ili kufikia usawa wa kijinsia, utekelezaji wake unahitaji mabadiliko makubwa katika jamii, elimu, utawala bora, na kubadilisha mifumo ya kijinsia ambayo imejengeka kwa muda mrefu.l, " ameeleza
Ameeleza kuwa faida za Bajeti yenye Mtazamo wa Kijinsia itasaidia kupunguza Tofauti za Kijinsia na kupunguza pengo kati ya wanawake na wanaume katika nyanja za kijamii, kiuchumi, na kisiasa ikiwa ni pamoja na kuongeza fursa za wanawake kupata elimu bora, huduma za afya, na kujiingiza katika shughuli za kiuchumi.
"Faida nyingine ni kuboresha Maisha ya Makundi ya Kijinsia,bajeti hii inajali mahitaji ya makundi yote ya kijinsia, ikiwemo wasichana, wavulana, na jamii zinazokumbwa na unyanyasaji au ukosefu wa haki, " amesema
Awali akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo Kaimu CAG Benja Majura ameeleza kufurahishwa kwake namna ambavyo MTANDAO huo unavyofanya kazi hasa katika katika masuala ya kijinsia na kueleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yatakuwa chachu kwenye kuongeza uelewa wa namna ya kuweka bajeti ya mlengo wa kijinsia.
No comments:
Post a Comment