Wanafunzi wa TASUBA wakiwakaribisha wageni kwa ngoma kabla ya mdahalo.
Mzee wa Mila wilayani Bwana Mwinyi Hashimu Akida akizungumza
Wadau wakisaini  ahadi ya kukuza Urithi wa Utamaduni Usioshikika mjini Bagamoyo 
Wadau wakifurahia ngoma
Na Mwandishi wetu, Bagamoyo
Wadau wanaofanya kazi za kudumisha Utamaduni wa Urithi Usioshikika wamesisitiza jamii kuendelea kuenzi michezo   ya asili  ili kutengeneza jamii ya watu wanaowajibika.
Michezo hiyo ukiwemo ule wa Baba na Mama   inaaminika kuwa ilisaidia makuzi ya mtu kujua majukumu yake kama mwanaume na mwanamke.
Ushauri huo ulitolewa mjini Bagamoyo wakati wa  mdahalo wa vijana uliolenga kuwajengea uwezo wa namna ya  kukuza Urithi wa Utamaduni Usioshikika katika nyakati hizi za kidijitali
Akichangia mjadala huu, bwana Anthony Tiluganilwa mdau kutoka TASUBA alisema michezo ya asili ilikuwa inawafundisha kujitegemea kwani walicheza nje bila wazazi na hivyo kudumisha upendo na watoto wengine tofauti na sasa ambapo watoto wengi wanafungiwa magetini.
“ Tulipocheza kama Baba na Mama, mwanamke aliigiza majukumu ya mama na wa kiume aliigiza majukumu ya Baba.  Jambo hili lilisaidia sana kwani hadi tumekua tunajua majukumu yetu.  Kwa sasa hili halifanyiki matokeo yake tuna watu  wabinafsi na wanaokwepa majukumu yao,” alisema Tiluganilwa.
Akichangia mjadala huo, mzee wa mila na mwenye ushawishi wilayani Bagamoyo bwana Hashimu Ally Kida alisisitiza umuhimu wa kukifundisha kizazi cha vijana ili kujua  tulikotoka.
“Ni vema tukaongeza juhudi za kujadiliana ili kizazi chetu kijue mila zetu na desturi ili kujua tulikotoka katika tamaduni zetu,” alisisitiza Mzee Akida.
Kwa upande wake Angela Kidwanga, mwanafunzi wa TASUBA alisisitiza umuhimu wa wazazi kuwafundisha Watoto kujitegemea ili kukwepa vijana kupenda mashangazi ( Wanawake waliowazidi umri) na mabinti kutafuta sponsors ( wanaume watu wazima) badala ya kufanya kazi.
“  Naomba niwashauri wazazi pia wawe wanawapeleka Watoto kijijini walikotoka ili wajue mila na utamaduni wao kuliko kuwaacha mijini.  Vilevile tunaomba watufundishe lugha zetu za asili badala ya kutumia Kiingereza tu,” alisema Kidwanga.
Urithi wa Utamaduni Usioshikika unajumuisha ujuzi na maarifa ya kiutamaduni katika jamii ikiwemo ujuzi wa kucheza ngoma za asili, kuandaa vyakula vya asili  na namna ya kujieleza ikiwemo lugha ambapo inasemekana lugha nyingi za asili zipo hatarini kupotea kutokana na wazazi kushindwa kurithisha kwa watoto wao.
Majadiliano haya yaliandaliwa na UNESCO kwa kushirikiana na serikali ili kuchagiza urithishwaji wa utamaduni usioshikika na namna ambavyo unaweza kuchagiza ajira  na kuongeza kipato  hususani katika nyakati hizi za kidijitali.

























No comments:
Post a Comment