DKT. SAMIA "ILANI YA UCHAGUZI ITAKAYOZINDULIWA NA CCM IMESHIRIKISHA MAKUNDI YOTE" - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 29, 2025

DKT. SAMIA "ILANI YA UCHAGUZI ITAKAYOZINDULIWA NA CCM IMESHIRIKISHA MAKUNDI YOTE"


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa mwaka 2025/2030 imeandaliwa kwa weledi mkubwa na kwa kushirikisha wananchi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii, asasi za kiraia, taasisi za elimu ya juu, pamoja na wadau wengine muhimu.

Akizungumza leo Mei 29, 2025 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, Dkt. Samia ameeleza kuwa kesho chama hicho kitazindua rasmi Ilani hiyo mpya ambayo itatumika katika kampeni za Uchaguzi Mkuu ujao.

Amebainisha kuwa lengo ni kuwaomba wananchi imani na ridhaa ya kukirudisha chama hicho madarakani kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Amefafanua kuwa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 ilikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mwelekeo wa sera za chama kwa kipindi cha miaka 2020 hadi 2030. Ilani ya mwaka huu, kwa upande wake, inaakisi awamu ya pili ya utekelezaji wa dira hiyo ya kisera.

“Kabla ya kuendelea mbele, tumeona ni muhimu kufanya mapitio ya utekelezaji wa Ilani ya miaka mitano iliyopita. Hiyo ndiyo kazi tutakayoifanya leo, na kesho tutaizindua rasmi Ilani mpya na kueleza yaliyomo ndani yake,” alisema Dk. Samia.

Aidha, ameeleza kuwa matarajio yake ni kwamba wajumbe wote wa mkutano huo watachukua jukumu la kuitangaza Ilani hiyo pamoja na mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2020/2025 kwa wananchi, kwa lengo la kujenga uelewa na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi.

Katika kuimarisha taasisi ya chama hicho, Dkt. Samia ametumia nafasi hiyo kuwajulisha wajumbe kuwa tarehe 28 Mei mwaka huu aliweka jiwe la msingi la makao makuu mapya ya CCM pamoja na ofisi zake, ikiwa ni ishara ya kuendeleza ujenzi wa taasisi imara ya kisiasa.

“Ninafurahi kuwaona wajumbe wote mkiwa na nyuso za bashasha. Nashukuru sana kwa mahudhurio yenu mazuri nyinyi pamoja na wageni wetu waalikwa. Nimepata mapokezi mazuri, nawashukuru sana wageni kwa kuungana nasi,” amesema Dkt. Samia

Ameongeza kuwa uwepo wa wageni waalikwa ni ushahidi wa mapenzi ya dhati ya kudumisha undugu, urafiki, umoja na mshikamano baina ya vyama vyao na wananchi wa mataifa yao.

Dkt. Samia pia amekumbusha kuwa katika Mkutano Maalum wa Januari 18 na 19, 2025, wajumbe walipokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za chama na jumuiya zake kwa kipindi cha 2020 hadi 2024, pamoja na taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katika mkutano huo, walipitisha marekebisho madogo ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, na kuidhinisha toleo jipya la mwaka 2020/2025. Vilevile, walimchagua Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara).

Kwa kuzingatia Ibara ya 100(2), 101(5)(b), na 103(4) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, Dkt. Samia alieleza kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, katika kikao chake cha Machi 10 mwaka huu, ilipokea na kuthibitisha Ilani ya uchaguzi ya mwaka huu, pamoja na kuwateua wagombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mgombea mwenza, na mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Amesisitiza kuwa mkutano huu ni sehemu ya maandalizi ya CCM kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

No comments:

Post a Comment