
OR - TAMISEMI
Serikali imetoa wito kwa wamiliki na waendeshaji wa vituo vya malezi na makuzi ya Watoto wadogo mchana kufuata taratibu,kanuni na miongozo ya uanzishwaji na uendeshaji wa vituo hivyo.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Ofisi ya Rais- TAMISEMI Shabani Muhali, baada ya kubaini baadhi ya vituo vya malezi na makuzi vya kuhudumia watoto wadogo mchana mkoani Kigoma kufanya shughuli za Malezi na Makuzo bila kuwa na miongozo ya serikali ya uanzishaji na uendeshaji wa vituo hivyo.
Akiongea kwa niaba ya timu maalum ya tathmini na ufuatiliaji shughuli za malezi na makuzi Ofisi ya Rais - TAMISEMI katika ziara maalumu ya ufuatiliaji na tathimini juu ya mwenendo wa utolewaji wa huduma za malezi na makuzi katika vituo hivyo, Shabani amesema timu hiyo imegundua mapungufu mengi ikiwa ni pamoja na walezi kutokuwa na elimu sahihi ya malezi huku baadhi ya vituo vikiendeshwa bila mwongozo maalum maarufu kama kiongozi cha Mlezi.
Kufuatia hatua hiyo Shabani amesema maelekezo ya serikali ni kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za malezi na makuzi kwa watoto wadogo mchana vinasajiliwa na kuendeshwa kwa kufuata miongozo maalum ili kutimiza dhamira njema ya uanzishwaji wa vituo hivyo.
Timu hiyo imekagua vituo mbalimbali vya kulelea watoto wadogo mchana katika wilaya za Kakonko na Kasulu Mkoani Kigoma na inaendelea na ziara yake Mkoani Mbeya, ikiwa ni kufanya ufuatiliaji na tathmini, na pia kutoa ushauri chanya katika kuboresha huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.




No comments:
Post a Comment